MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Saturday, 29 December 2018

DC Moses Machali akabidhiwa kinyago cha Masikitiko


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amekabidhi kinyago cha huzuni kwa viongozi wa wilaya ya Nanyumbu kufuatia kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa kwa darasa la saba  mwaka 2018.

Kinyago hiki chenye lengo la kuhamasisha ushindani wa kielimu kwa halmashauri za mkoa wa Mtwara kwa ngazi zote kimetolewa mbele ya wajumbe wa kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mtwara Disemba 28, 2018.

Awali wakijadili mbinu za kuhamasisha ushindani wa kimasomo kwa wanafunzi wa ngazi zote ndani ya mkoa wajumbe walikubaliana kuweka utaratibu wa kuzungusha kinyago hicho kinachomuonesha baba na mama wakiwa katika simanzi na majonzi makubwa.

 Mheshimiwa Byakanwa amesema licha ya Nanyumbu kupokea kinyago bado wanajukumu la kuongoza kikao cha wadau wa elimu mkoa kitakachofanyika mapema mwaka 2019  ambapo pamoja na mambo mengine watatakiwa kuwaambia wajumbe ni kwa nini wamekuwa wa mwisho na mikakati gani waliyo nayo kujitoa katika nafasi hiyo.

Akizungumza baada ya kupokea kinyago hicho, Mbunge wa jimbo la Nanyumbu Mheshimiwa Dua William Nkurua amesema wamepokea kinyago hicho kwa mikono miwili na kwamba kitawasidia kujitafakari na kuongeza juhudi ili kujitoa katika aibu hiyo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Moses Joseph Machali amesema wanaenda kujipanga ili kuhakikisha kinyago hicho kinakabidhiwa wilaya nyingine mwaka ujao. Amesema zipo changamoto nyingi ambazo wamezianisha ikiwemo upungufu wa walimu, utendaji kazi usioridhisha pamoja na miundombinu mibovu.

“Tutahakikisha changamoto zote tunazitatua ili mwakani kinyago hiki kichukuliwe na wilaya nyingine”. Amesema Machali

Kwa upande wake mwakilishi wa gazeti la Habari leo Mkoa wa Mtwara Sijawa Omary amepongeza maamuzi ya kikao hicho ya kuizawadia kinyago halmashauri iliyoshika nafasi ya mwisho kwa ufaulu kwenye mitihani ya darasa la saba.

“Uamuzi huo ni mzuri kwani unahamasisha ushindani. Wanachotakiwa kufanya sasa ni kukipa jina ambalo litakuwa na mtazamo wa mkoa wa Mtwara. jina ambalo litawafanya wamiliki wake kuhuzunika kweli” Amesema Sijawa.

Tangu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa huu mapema mwaka huu ameahidi kuhakikisha elimu ya mkoa wa Mtwara inainuka ambapo mafaniko yake yameanza kuonekana.
Mwaka 2018 mkoa umekuwa katika nafasi ya nane kitaifa kutoka nafasi ya 22 katika matokeo ya darasa la Saba mwaka 2017 huku ukishika nafasi ya kwanza katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment