Na; Herieth Joseph Kipuyo - Afisa Lishe, Evaristy Masuha-Afisa
habari.
(Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara)
Kwa
wasomaji wapya. Hii ni sehemu ya tatu ya makala zinazozungumzia Lishe ya jamii. Wiki iliyopita tulizungumzia aina
za kisukari na namna mgonjwa wa kisukari anavyoweza kudhibiti vyakula vyenye
asili ya nafaka, mizizi na ndizi ili visiongeze sukari kwa wingi kwenye
damu. Leo tunaendelea kuzungumzia namna mgonjwa wa kisukari anavyoweza kula
vyakula kutoka katika makundi mengine ya vyakula. Tuwe pamoja.
Vyakula asili ya wanyama na vyakula
jamii ya kunde. Vyakula jamii ya kunde vina makapimlo kwa wingi (nyuzinyuzi)
hivyo mgonjwa wa kisukari anashauriwa kutumia zaidi kama kitoweo na ale
tofautitofauti mfano maharage, kunde, njegere, mbaazi, njugu, choroko n.k. Anashauriwa kupunguza matumizi ya nyama
hususani nyama nyekundu na kama italiwa isizidi nusu kilo kwa wiki. Apendelee zaidi samaki na kuku (kuku aondoe
ngozi) ila ale kulingana na mahitaji ya mwili wake kuepuka uzito mkubwa wa
mwili.
Mbogamboga. Mgonjwa anatakiwa kula mbogamboga kwa wingi. Mgonjwa ale mbogamboga tofautitofauti. Mboga za majani zisipikwe bila mafuta kabisa bali zipikwe kwa kiasi kidogo cha mafuta ili virutubishi vyote viweze kufyozwa vyema mwilini. Mbogamboga zikipikwa bila mafuta virutubishi havita weza kufyonzwa mwilini ipasavyo na hivyo mgonjwa anaweza kupata matatizo mengine ya kilishe. Mfano wa mboga mboga ni mchicha, chainizi, matembele, spinachi, kisamvu, biringanya, bamia, nyanya chungu, kabichi, hoho, n.k. mboga za majani zenye rangi ya kijani ni muhimu kwani ina wingi wa madini ya manganese ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa kichocheo cha insulini.
Matunda. Kula matunda freshi kiasi kidogo kwa kila mlo
mfano embe saizi ya kati, chungwa saizi ya kati, ndizi moja ndogo, kipande cha
papai, nanasi, tikiti n.k. (tunda usawa wa ngumi moja kwa kila mlo). Kiasi
kikubwa cha sukari iliyopo kwenye matunda ni fructose ambayo haihitaji insulini
katika kumeng'enywa. Tumia zaidi matunda
kuliko juisi ya matunda na ikiwezekana
tumia matunda na maganda yake bila kumenya mfano. embe, epo n.k. chungwa
kula na makapi meupe ya ndani. makapi mlo katika matunda (nyuzinyuzi) husaidia
kupunguza kasi ya ufyonzwaji wa sukari mwilini.
Matunda
Vyakula asili ya Sukari, Mafuta na
asali. Katika kundi hili epuka sukari na vyakula vyenye sukari nyingi kama
soda, pipi, chokoleti, asali, jamu, biskuti na keki. Mwili huchukua muda mfupi sana
kuyeyusha vyakula hivi na hivyo kasi ya kuongeza sukari kwenye damu inakuwa
juu. Tumia kiasi kidogo cha mafuta wakati wa kupika na pendelea zaidi mafuta ya
mimea kama alizeti, ufuta, nazi, karanga, korosho n.k. Mgonjwa wa kisukari yupo
katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo na shinikizo kubwa la damu hivyo
aepuke vyakula vyenye mafuta kwa wingi. Mgonjwa asiache kabisa kutumia mafuta.
Kutokana na aina ya makundi makuu matano ya vyakula yaliyoainishwa hapo
juu, unashauriwa kuchagua chakula kimoja kutoka kila kundi ili uweze kula mlo
kamili. Zingatia maelekezo yaliyotolewa katka kila kundi.
KUMBUKA : Mgonjwa
wa kisukari hahitaji kula chakula maalumu tofauti na wanafamilia wengine, isipokuwa
mlo wake ni lazima uwe na mbogamboga kwa wingi na matunda kwa kiasi kidogo. Pia
mlo uwe na nafaka zisizokobolewa kwani ni chanzo kizuri cha makapi mlo
(nyuzinyuzi). Makapi mlo yanachukuwa muda mrefu kusagwa tumboni hivyo kufanya sukari mwilini kutoongezeka
haraka.
KUMBUKA : Wewe
ni nguzo muhimu katika kumudu ugonjwa huu. Tafuta ushauri wa kitaalamu,
usikubali kudanganywa na watu wasiokuwa na uelewa mzuri kuhusu ugonjwa huu. Jiunge
na kiliniki ya kisukari ili uendelee kuimarisha Afya yako.
Usikose makala ijayo ambayo itazungumzia
mambo ambayo mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuzingatia sambamba na ulaji.
nakala hii ni nzuri na nimejifunza mengi saana
ReplyDeleteNimeelewa viz
ReplyDeleteMbarikiwe kwa kuendelea kuelimisha watu
ReplyDeleteAsante sana...
ReplyDeleteFrom mtwara