MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Sunday 14 November 2021

Naibu Waziri Mahundi atembelea Bwawa la Nyerere.

 Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ametembelea mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa lengo la kukagua namna uongozi wa Bonde la Mto Rufiji wanavyosaidia kulinda vyanzo vya maji vinavyoingiza maji katika bwawa hilo.

Ziara hiyo imefanyika jana Novemba 13, 2021 akiambatana na Mwenyeji wake Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, Mhandisi Florence Mahay. 

Mhe.  Mahundi amepongeza jitihada kubwa zinafanywa kuhakikisha mazingira ya Bonde la Mto Rufiji yanakuwa salama.

Aidha,  ameagiza wadau wote wa maji katika maeneo yanayozunguka bwawa hilo kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mazingira ya vyanzo vya maji katika eneo linalozunguka mradi huo yanakuwa salama.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Maji inaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha miradi iliyokusudiwa inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Ziara ya Mhandisi Mahundi kutembelea mabonde yanayochangia maji kwenye mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ilianzia mkoa wa Njombe, Iringa, Mbeya na kuhitimishwa mkoani Morogoro.











Friday 8 May 2020

wanaopandisha bei ya sukari wakamatwa Mtwara

Serikali ya Mkoa wa Mtwara imeanzisha operation maalumu ya kuwakamata wafanyabiashara wanaouza sukari kinyume na maelekezo ya serikali. Zoezi hilo lililoanza jana limeweza kuwakamata wafanyabiashara wanane ambao walikutwa wanauza sukari kwa bei ya hadi shilingi 3600 kwa kilo moja.

Akizungumza mara baada ya kumuapisha Mhe. Dunstan Kyobya aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa amesema operation hiyo ni endelevu kwa mkoa mzima. Amewataka wananchi watowe taarifa kwa jeshi la polisi juu ya wafanyabishara wanaokiuka maagizo.

maelezo zaidi fungua hiyo video au tembelea youtube channel ya Mtwara RS. Usisahau kusubscribe huko.

Friday 17 April 2020

Wachina wajitosa kusapoti mapambano dhidi ya CORONA Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa ametoa wito kwa Taasisi, Mashirika na watu binafsi wenye uwezo wa kutengeneza barakoa (Mask) watengeneze kwa wingi.  Wito huo ameutoa leo Aprili 17, 2020 wakati akipokea msaada wa vifaa vya kujikinga na maradhi ya COVID-19 kutoka kwa kampuni ya Beijing Construction and Engineering Group CO. LTD inayoshughulika na upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Mtwara.

Amesema mahitaji ya vifaa hivyo kwa sasa ni makubwa hasa kwa watoa huduma na watu wote ambao kila siku wanafanya kazi ya kukutana na watu. Aidha, amesisisitiza jamii kuendelea kujikinga na ugonjwa huo kwa kuzingatia tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa huku akiwasisitiza wageni wanaotembelea ofisini kwake kuhakikisha wanavaa barakoa.

“..na mimi kama Mkuu wa Mkoa, tutakapoanza wiki inayofuata, hakuna mtu atakayefika kwenye ofisi yangu bila kuvaa Mask. kuanzia jumatatu tarehe 20, kila mtu atakayefika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa atapaswa kuwa amevaa Mask.” Amesema Byakanwa.

Naye  Meneja wa kampuni  ya Beijing  Construction Cui Rui Tao ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa hatua inazochukua dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. Amesema wameona umuhimu wa kusaidia jitihada hizo kwa kutoa msaada wa Barakoa elfu moja,  galoni 10 za lita tanotano Pamoja na vitakasa mikono.

 Kutazama video ya makabidhiano. Bonyeza hapo. https://www.youtube.com/watch?v=CQXKWDd3r7E

Tuesday 7 April 2020

Kondakta watakiwa kuzingatia afya ili kujikinga na Korona



Mkuu wa mkoa wa Mtwara amewataka madereva, kondakta na wakatisha tiketi wa magari ya abiria yanayoingia na kutoka Mkoani Mtwara kuzingatia misingi ya afya ili kujilinda  wenyewe pamoja na abiria, dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Agizo hilo amelitoa leo Aprili 7, 2020 wakati akizindua mpango wa upuliziaji dawa magari ya abiria kwa mkoa wa Mtwara zoezi ambalo litafanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja. Katika uzinduzi huo uliofanyika kituo cha mabasi cha Chipuputa Manispaa ya Mtwara Mikindani amesisitiza wapiga debe wasiwavute abiria na mizigo yao kwani ni kero na hatari kwa kipindi hiki cha maambukizi ya CORONA.
 
“Kilichonisikitisha sana, wamiliki wa magari hamjaongea na wafanyakazi wenu. Sikutegemea niwe stendi, nishuhudie konda au mkatisha tiketi anagombea abiria, anamshika mkono…. Huyo abiria mkaribishe tu hakuna kushikana wala kubebeana mizigo.” Amesema Byakanwa.  

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sylivia Mamkwe amesema zoezi hilo litafanyika kwa standi zote za wilaya za mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha mwezi mzima huku Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Kanali Emmanuel Mwaigobeko akisema wamejipanga kuhakikisha standi kuu za magari na daladala zote za ndani ya manispaa zinatekeleza zoezi hilo.
Sylivia Mamkwe. Mganga Mkuu wa Mkoa akizungumza na waandishi wa Habari
Mkurugenzi Manispaa Mtwara Mikindani Kanali Emmanuel Mwaigobeko akinawa mikono kabla ya kuingia ,ndani ya eneo la kituo cha mabasi Chipuputa

“Upuliziaji huu utakuwa ukifanyika kila siku asubuhi kwa standi zetu zote za Manispaa ikiwamo standi ya zamani, Standi kuu ya Chipuputa, na standi ya daladala iliyoko Mikindani”. Amesema Mwaigobeko.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara, Nassoro Mansoor Hassan ameishukuru serikali kwa kusimamia zoezi hilo na kusema limegharamiwa na wamiliki wa mabadi kwa kusimamiwa na serikali. Aidha wataendelea kuchukua hatua zaidi kadiri watakavyokuwa wakipokea maagizo kutoka serikalini.
Nassoro Mansoor Hassan. Mwenyekiti Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara 

“Lengo letu ni kuhakikisha sisi na abiria wetu tunakuwa salama hivyo tutachukua hatua kadiri serikali itakavyotuongoza” Amesema Nassoro

Monday 6 April 2020

Sirro awahakikishia ulinzi wakazi Mtwara







Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IGP) Simon Sirro
amewahakikishia ulinzi na usalama wananchi wa mkoa wa Mtwara na kuwataka wafanye
kazi zao bila hofu yoyote. Ameyasema hayo leo Aprili 6, 2020 wakati wa ziara ya
viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini yenye lengo la kuangalia
namna walivyojipanga kukabiliana na uhalifu ndani ya nchi na mipakani.

“kitendo cha kuona wanakuja wanachinja watu
wetu lazima ifike mahali tuseme mwisho na iwe mwisho. Wao wametangaza ligi. Wametangaza
mapambano lazima na sisi tuwe tayari kwa mapambano”. Amesema Sirro.

Bonyeza hapo chini usikilize

Monday 30 March 2020

Polisi waimarisha ulinzi mpka wa Tanzania-Msumbiji







Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama Vimeimarisha ulinzi katika mipaka ya Tanzania ili kuhakikisha
wahalifu wanaofanya mauaji na vurugu nchini Msumbiji hawapati nafasi ya kuingia
Tanzania. 

Hayo yamesemwa leo na Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo wa Jeshi la Polisi Liberatus Sabas wakati akikagua kikosi maalumu cha
kupambana na uhalifu nchini kilichowasili mkoani Mtwara kwa ajili ya kuimarisha
ulinzi katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji. 
 
Amesema wahalifu hao wamekuwa wakivamia  kambi za jeshi, vituo vya polisi, kuchoma
moto na kuchukua silaha nchini Msumbiji na pia wameripotiwa kuvamia benki na
kupora fedha huko huko Msumbiji.

“Kule hali si shwali kama ambavyo mmekuwa mkisikia
kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Sisi kwa kutambua hilo, na kutambua
umuhimu wa sisi kama Taifa, na umuhimu wa wananchi wa Tanzania kuwa shwali
tumejipanga kuhakikisha tatizo hili haliji huku kwetu.”

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwasilisha
taarifa za mtu yeyote ambaye wanamtilia shaka.