MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Friday 19 April 2019

Ulaji unaofaa kwa mgonjwa wa Kisukari


Na; Herieth Joseph Kipuyo, Evaristy Masuha 

Kwa wasomaji wapya. hii ni sehemu ya pili ya makala zinazozungumzia Lishe  ya jamii. Wiki iliyopita tulizungumzia ulaji unaofaa kwa ujumla.  Leo tunakuletea ulaji unaofaa kwa mgonjwa wa kisukali. 

Makala hizi ambazo zinakujia kila jumamosi zinatokana na ukubwa wa tatizo la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaweza kuzuiwa kwa kuishi kwa kufuata mtindo bora wa maisha.
Makala hizi zinaletwa kwenu na   Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara, Herieth Joseph Kipuyo, Afisa lishe pamoja na Evaristy masuha, Afisa Habari.

Endelea..

Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na chakula huhitaji kichocheo cha insulini ambacho hutengenezwa na kongosho kwa lengo la kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Kongosho inaposhindwa kutengeneza kichocheo cha insulini au insulini iliyopo katika damu inaposhindwa kufanya kazi kwa ufanisi husababisha ugonjwa wa kisukari.

Kuna aina kuu mbili za kisukari ambazo ni kisukari kinachotegemea insulini (type 1 diabetes) na kile kisichotegemea insulini (type 2 diabetes).
   Kisukari kinachotegemea insulini (type 1 diabetes) huwapata zaidi watoto na watu wenye umri chini ya miaka 35.
    Kama kuna kiashiria cha historia ya ugonjwa huu katika familia ni bora kuwa makini sana na kufuata mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji unaofaa (WHO, 2018).

    Mambo mengine yanayoongeza hatari ya kupata aina hii ya kisukari kwa mtoto
  • Mtoto kupewa maziwa mbadala (ya kopo au ya wanyama tofauti na maelekezo ya ulaji wa watoto wachanga na wadogo) au kumnyonyesha mtoto kwa muda mfupi. Inashauriwa mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila kitu kingine chochote (hata maji) katika miezi sita ya mwanzo. Baada ya miezi sita aendelee kunyonyeshwa na kupewa chakula cha nyongeza hadi atimize miaka miwili au zaidi.
  • Mtoto akizaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi
  • Unene au uzito mkubwa utotoni. Hii husababishwa na ulaji mbovu usiozingatia kanuni za ulaji wa watoto wadogo na wachanga.
Kisukari kisichotegemea insulini (type 2 diabetes) huwapata zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea. Aina hii ya kisukari  huhusishwa kwa kiasi kikubwa na mtindo wa maisha usiofaa  (WHO, 2018).
Hata hivyo aina ya kisukari huthibitishwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa kufanyiwa uchunguzi sambamba na tiba sahihi.

MAPENDEKEZO YA ULAJI KWA MGONJWA WA KISUKARI
·  Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku kwa kuzingatia muda  uliyojipangia sambamba na milo midogo midogo angalau mara mbili.  Mfano wa milo midogo midogo ni kikombe cha maziwa fresh/mtindi, kipande cha mahindi iliyochomwa/chemshwa, karanga, korosho n.k. Usikae na njaa muda mrefu kwani sukari itashuka.
Mlo kamili ni chakula chenye mchanganyiko wa makundi yote makuu matano ya vyakula angalau chakula kimoja kutoka katika  kila kundi ambayo ni  
  • Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi,
  •  Vyakula vya jamii ya wanyama na jamii ya mikunde, 
  • Mbogamboga
  • Matunda na
  • mafuta.
Vyakula vya asili ya nafaka, mizizi na ndizi . 
Katika kundi hili la nafaka, mizizi na ndizi mgonjwa wa kisukari anashauriwa kupendelea zaidi vyakula visivyokobolewa mfano. ngano isiyokobolewa, dona, mtama usiokobolewa n.k. ila viandaliwe kwa kuzingatia usafi na usalama wa chakula ili kuepuka sumu kuvu. 
Vyakula visivyokobolewa huwa na makapi mlo kwa wingi (nyuzinyuzi) ambayo mwili huchukua muda mrefu kuyeyusha na hivyo kasi ya kuongeza sukari kwenye damu hupungua. Aidha, mgonjwa anashauriwa kula vyakula hivyo kwa kiasi kidogo (ngumi moja) sambamba na mboga za majani au jamii ya kunde kwa wingi ili kuongeza makapi mlo yatakayosaidia kudhibiti kasi ya sukari kuongezeka kwenye damu.
                               Vyakula jamii ya kunde  
                                                                               Mbogamboga 

Endapo mgonjwa atakula vyakula visivyo na makapi mlo kwa wingi kama ndizi, mihogo, viazi, wali wa kawaida, n.k. anashauriwa kula kwa kiasi kidogo sana sambamba na vyakula vyenye makapi mlo (nyuzinyuzi) kwa wingi  sana ili isaidie kupunguza kasi ya sukari kuongezeka  kwenye damu. Makapi mlo hupatikana katika vyakula vya jamii ya kunde kama kunde, maharage, njegere, mbaazi n.k. na mbogamboga kama mboga za majani, matango, nyanya, hoho, biringanya, bamia, nyanya chungu n.k. 
Mgonjwa wa kisukari hashauriwi kuacha kabisa kula vyakula vya wanga ila azingatie maelekezo hapo juu. 

Usikose makala ijayo ambayo itaendelea kuzungumzia ulaji unaoshauriwa kwa mgonjwa wa kisukari kwa makundi mengine ya vyakula ambayo ni jamii ya wanyama na mikunde, mbogamboga, matunda na mafuta.



No comments:

Post a Comment