MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Tuesday, 28 August 2018

Ijuwe Lumesule. Lilikopiganwa pigano la mwisho la vita ya majimaji.Na, Evaristy Masuha
Vita ya majimaji ilianza Julai 1905 na kumalizika Januari 1907. Pigano la kwanza lilianzia mkoani Lindi katika kijiji cha Nandete wilayani Kilwa likiongozwa na Mzee wa kimatumbi aliyejulikana kwa jina la Kinjekitile Ngwale. Miezi miwili baadaye Kinjekitile alikamatwa na Kunyongwa hadi kufa.

Pigano la mwisho lilifanyika katika kijiji cha Lumesule kilichoko wilayani Nanyumbu mkoa wa Mtwara likiongozwa na kiongozi wa wangindo, Abdallah Mapanda.

Kijiji hiki kiko katika mpaka wa Wilaya ya Nanyumbu iliyoko mkoani Mtwara na Wilaya ya Tunduru iliyoko mkoani Ruvuma.
Jambo kubwa linaloitofautisha Lumesule na vijiji vingi vilivyopigana vita ya majimaji ni kulinda uhalisia ya mazingira ya nyakati za mapigano ya vita ya majimaji.
Wapiganaji wa vita ya majimaji
Nyakati za vita ya Majimaji sehemu kubwa ya mikoa ya kusini ilikuwa ni mapori yenye wanyama wakali. Wanyama hao ni moja ya sifa iliyomfanya mganga maarufu wa kijiji cha Ngalambe huko Kilwa Mzee Kinjekitile Ngwale kuaminiwa na wananchi wote wa mikoa ya kusini.

Ushahidi huu unapatikana kupitia maandiko ya waandishi mbalimbali akiwemo John Iliffe kwenye kitabu chake ‘A modern History of Tanganyika’ pamoja na Fr. Elzear Ebner katika kitabu chake ‘The History of Wangoni.’ Wawili hawa wanasema Kinjekitile alikuwa na mifugo mingi ikiwemo Simba na chui. Uwezo wa kufuga wanyama hao pamoja na uwezo wake wa uganga wa asili ulifanya dunia ya mikoa ya kusini iamini taarifa yake ya kugundua dawa ya kubadili risasi za Wajerumani kuwa maji kwa kutamka neno la kimatumbi ‘Mase’ ambalo maana yake kwa Kiswahili ni Maji.  

 
Msitu wa Lukwika-Lumesule
Miaka zaidi ya mia moja baadaye sehemu pekee katika mikoa ya kusini ambako unaweza kuwaona simba, chui, na wanyama wengine wenye sifa sawa na simba wa Kinjekitile ni katika msitu wa hifadhi ya kijiji cha Lumesule ambayo imeungana na kijiji jirani cha Lukwika. (Hifadhi ya wanyama ya Lukwika-Lumesule). Simba wa Lukwika-Lumesule hawajafugwa lakini ni wapole kama simba wa Kinjekitile.

Pia mita kadhaa kutoka Lumesule unaweza kuuona mlima wa Makong’ondela ambao una mapango makubwa ambayo ndani yake panaaminika kuwemo mafuvu ya binadamu. Zipo simulizi nyingi juu ya chanzo cha mafuvu haya lakini Wengi wanayahusisha na wahanga wa vita ya majimaji ambayo zaidi ya waafrika 75,000 wanatajwa kuuawa katika maeneo mbalimbali kulikopiganwa vita hii.

 Licha ya simba na mafuvu hayo bado yupo nyani muongoza watalii ambaye anapatikana katika mlima wa Mahinyo ulioko kijijini Chivilikiti kilometa kadhaa kutoka Lukwika. Nyani huyu mpole amekuwa kivutio kwa wageni kutokana na ukarimu wake wa kupokea mizigo ya wageni na kuwaongoza katika maeneo mbalimbali ya mapango ya mlima huo.
Afisa Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Raphael Mputa akisalimiana na Nyani Muongoza Watalii kabla ya kuanza ziara ya kutemblea mapango
Pamoja na ukweli kwamba sehemu kubwa ya kumbukumbu ya vita ya Majimaji inapatikana huko Songea bado wageni wanaotembelea kumbukumbu hizo hasa waliosoma vizuri historia hupata muda wa kutembelea Lumesule kujionea simba wa Kinjekitile na nyani wa Mahinyo.
Ukiachilia mbali umaarufu wa kihistoria wa kijiji cha Lumesule ambacho sehemu kubwa ya wakazi wake ni Wamakua, kijiji hiki ni moja ya vijiji ambavyo ni maarufu katika uzalishaji wa zao la korosho kikiungana na vijiji vingine vya mkoa wa Mtwara katika uzalishaji wa zao hili muhimu katika uchumi wa mkoa wa Mtwara. Nyani muongoza watalii akipata chakula baada ya shughuli ndefu ya kuongoza watalii 
Kama walivyo wananchi wengine wa Mkoa wa Mtwara wamakua wa Nanyumbu pia hutumia kaulimbiu ya ‘Mtwara Kuchele’ wakimaanisha Mtwara Kumekucha. Kaulimbiu hii hutumika mara nyingi katika kutambulisha maendeleo waliyoyafikia katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. 
Kwa kutambua fursa mbalimbali za utalii zilizoko wilayani Nanyumbu Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Moses Machali aliyeteuliwa kuongoza Wilaya hiyo hivi karibuni ameahidi kuifanya Nanyumbu Kuchele kwelikweli. Moja ya mikakati yake ni kuhakikisha fursa zote za utalii wilayani Nanyumbu zinatambulishwa duniani kote. 
No comments:

Post a comment