MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Wednesday 25 July 2018

Sababu za mkoa wa Mtwara kuwa wa kwanza kitaifa kidato cha Sita 2018 hizi hapa


 
Walimu Wakuu wa shule za Kidato cha Sita Mkoani Mtwara wakiwa na vyeti vya pongezi walivyokabidhiwa na Mhe. Mkuu wa Mkoa kutokana na kuwezesha mkoa kuwa wa kwanza katika matokeo ya kidato cha sita 2018. waliokaa ni viongozi wa mkoa wa Mtwara wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (wa Nne kutoka kushoto)

Umoja na mshikamano kati ya walimu, wanafunzi, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa Elimu umetajwa kuwa sababu kuu ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha sita mkoani Mtwara. Umoja huo umewaimarisha na kuwatia moyo walimu na wanafunzi katika kutatua changamoto mbalimbali za kielimu hatimaye kuufanya mkoa wa Mtwara kuwa wa Kwanza katika mitihani ya kidato cha sita kitaifa mwaka 2018. 
 
Mkuu wa Mkoa akimvalisha Medali Maalumu Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandahimba Moses Mathias shule ambayo imekuwa ya kwanza kimkoa na kushika nafasi ya 27 kitaifa matokeo ya kidato cha Sita 2018
Hayo yamesemwa leo na walimu wa shule mbalimbali za kidato cha tano na sita mkoani Mtwara wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa kwa lengo la kuwapongeza walimu hao.

Akifafanua misingi ya umoja huo Mwalimu Hansi Kipamila wa shule ya sekondari Tandahimba ambayo imekuwa ya kwanza kimkoa na kushika nafasi ya 27 kitaifa amesema shule imeweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa elimu ambayo imewezekana kutekelezwa kutokana na umoja na mshikamano.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani ya ndani (Moderation), mitihani ya majaribio kwa kila wiki pamoja na mitihani ya ushirikiano kati ya shule hiyo na shule ya sekondari Kiuta iliyoko katika wilaya hiyo.

Mikakati mingine ni motisha kwa walimu na wanafunzi ambayo hutolewa na Mkuu wa shule pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo jambo ambalo limeongeza morali ya kufundisha na kujifunza kwa wanafunzi. 

Amesema wakati mwingine walimu wa masomo ya pamoja hushirikiana kuingia madarasani ili kutatua changamoto za wanafunzi kwa pamoja. 

 
 Mwalimu Gasper Wechande
Naye mwalimu Gasper Wechande wa shule ya sekondari Kiuta amesema utaratibu wa kumaliza mitaala mapema umewasaidia kwani hupata muda mrefu wa kufanya majaribio ambayo husaidia kugundua kasoro za mwanafunzi mmoja mmoja. Pia huwagawanya wanafunzi wanaopata ufaulu wa chini na wale wanaopata ufaulu wa juu ambapo wale waliopata ufaulu wa chini hupewa muda wa ziada katika makundi yenye walimu wa kuwasimamia ili waendane na wenzao.

 
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara, Paul Kaji akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa
Aidha mwalimu Mkuu wa Shule ya Ufundi ya Mtwara, Mwl. Paul Kaji ameeleza kuwa njia nyingine ambayo imekuwa msaada katika kufanikisha matokeo mazuri kwa wanafunzi wa shule yao ni mtihani maalumu wa kuwajengea kasi ya kumaliza mtihani kwa wakati. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amewapa vyeti vya pongezi shule zote zilizofanya vizuri na kuwataka waendelee na jitihada hizo kupitia kauli mbiu aliyoitambulisha kwa lengo la kuwataka watokomeze ufaulu wa daraja la sifuri. “Mtwara is a zero free zone in form six results, Play your part”.

Ameagiza kila shule ihakikishe inalenga wanafunzi kufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu. Amesema hilo linawezekana kwani mfano mzuri umeonekana katika matokeo ya mwaka huu ambapo wanafunzi 1,020 kati ya 1499 wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la pili. Aidha ametoa pongezi maalumu kwa shule za serikali kuongoza kwa nafasi ya kwanza hadi ya 5 katika mkoa. Amesema hilo ni jambo la kujivunia kwani hayo ni mageuzi makubwa ya Elimu mkoani.

 
 Awali akisoma matokeo ya ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka 2018 Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara Germana Mung’aho amesema ufaulu wa kidato cha sita kwa mwaka 2018 Mkoa wa Mtwara umekuwa wa kwanza kati ya mikoa 29 ya Tanzania.
Nafasi hiyo imefikiwa baada ya watahiniwa wote 1499 waliofanya mtihani huo toka Mkoani Mtwara kufaulu kwa asilimia mia. Aidha  wanafunzi 11 tu ndio wamefaulu kwa daraja la Nne huku wengine wote wakiwa wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.
 
 Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara, Germana Mung'aho (Wa sita toka kulia waliosimama) akiwa pamoja na walimu wa kidato cha tano na sita pamoja na baadhi ya viongozi wa elimu mkoani Mtwara baada ya walimu hao kukabidhiwa vyeti vya pongezi.

1 comment: