MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Tuesday, 30 October 2018

Hongera Mtwara Ukombozi wa elimu tumeuona


Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akisalimiana na wanafunzi wa shule ya Sekondari Aquinas alipowasili shuleni hapo katika hafla fupi ya kupongezana mara baada ya matokeo ya kidato cha sita 2018 ambapo mkoa wa Mtwara uliongoza kitaifa

Methali moja ya kihaya inasema ‘Abachumita Empunu Bema Lubaju Lumo’. Tafsiri ya kiswahili ni kwamba wachomao mkuki nguruwe pori, hukaa upande mmoja. Methali za Kiswahili zinazofanana na msemo huu ni umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Kichango huchangizana. Wafanyao kazi inayofanana, hunia mamoja.

Methali hii inatafakari kubwa katika njia tuliyoianza kama mkoa. Tumepiga hatua ndefu ya mapambano dhidi ya adui ujinga. Hatua hii ndiyo imetufikisha katika nafasi ya nane kati ya mikoa 26 katika matokeo ya darasa la saba 2018 kutoka nafasi ya 22 mwaka 2017.

Takwimu za nyuma si njema sana kwa mkoa kwani mwaka 2015 mkoa ulishika nafasi ya 12 wakati Mwaka 2016 ulishika nafasi ya 25.

Mafanikio haya huwezi kuyatenganisha na matokeo ya kidato cha sita 2018 ambapo mkoa umekuwa wa kwanza katika mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.
Tunaweza kuainisha sababu nyingi za ufaulu lakini hatutaacha kusema umoja na mshikamano kati ya viongozi na wadau wa Elimu mkoani Mtwara umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio haya.

Umoja huu ndio unatoa nafasi ya pongezi nyingi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa Kwa jitihada zake tangu alipopewa nafasi ya kuongoza mkoa huu Oktoba 26 mwaka jana.

Jitihada hizi zilianza kuonekana tangia vikao vyake vya awali na wadau wa Elimu ikiwemo kikao maalumu cha kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichotoka na mikakati mbalimbali aliyoahidi kuisimamia.

Jitihada hizi ni pamoja na zile zilizobainisha shule 10 ndani ya halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambazo wanafunzi wake walikuwa wakisomea kwenye mikorosho. Wadau kwa pamoja wakamuunga mkono kwa michango mbalimbali hatimaye leo hii watoto wanasomea kwenye madarasa mazuri ya kisasa.

Jitihada hizi ndizo zilizoagiza wanafunzi na walimu wote wanaoacha alama ya mafanikio shuleni kwao kutambuliwa kwa utaratibu maalumu wa vibao wa wazi kama motisha kwa wengine. Ni jitihada hizihizi zilizoagiza walimu kumaliza mtaala mapema mwezi Juni ili kuwapa muda wanafunzi kufanya majaribio na marudio.

Kwa mikakati hii nakubaliana na baadhi ya wadau walioandika sehemu mbalimbali kukubaliana na mikakati ya mkoa akiwemo aliyewahi kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za  Mitaa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara vijijini Mheshimiwa Hawa Ghasia ambaye aliandika kwenye kundi la whatsap la viongozi wa mkoa. (Mtwara Leaders Group)

“Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Byakanwa, viongozi na watendaji wa ngazi zote kwa kuwezesha mkoa wa Mtwara kushika nafasi ya Nane kitaifa. Ushirikiano, mshikamano na usimamizi madhubuti chini ya uongozi wako matunda tumeanza kuyaona haraka kuliko tulivyotarajia”
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gelasius Byakanwa akishiriki ujenzi wa shule ya Msingi Mitambo. Hii ni moja kati ya shule kumi ambazo wanafunzi wake walikuwa wakisomea chini ya Mikorosho.

Inawezekana kabisa alikosekana wa kutukalisha Lubaju lumo (upande mmoja) dhidi ya mila na tamaduni zinazokwamisha elimu kwa mikoa ya kusini.

Inawezekana alikosekana wa kutukalisha lubaju lumo katika mapambano dhidi ya mimba shuleni.

Inawezekana tulishindwa kuwa pamoja katika kuwasimamia walimu kutimiza wajibu wao. inawezekana tulishindwa kuwa lubaju lumo katika kumuwezesha mtoto afahamu nia njema ya mzazi kumpeleka shule.

Hisia hizi zinakumbusha moja ya maneno ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. William Ole Nasha wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa pamoja na Wakuu wa shule za sekondari za kidato cha sita mkoani Mtwara katika ukumbi wa shule ya sekondari ya ufundi Mtwara mara baada ya matokeo ya kidato cha sita kitaifa 2018. Mheshimiwa Nasha alisema.

“Hakuna kinachoitwa kufaulu kwa coincidence. Haitokei bahati mbaya. Panapoufaulu kuna jitihada, kuna uongozi, kuna watu wamefanya kazi. Ndiyo maana nafurahi kuja kukutana na ninyi viongozi wa mkoa na wakuu wa shule za sekondari za kidato cha sita mkoa wa Mtwara kuwaambia mmefanya kazi nzuri.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. William Ole Nasha  akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ufundi Mtwara. (hawapo pichani)
Huu ndio ukweli usiopingika kwamba viongozi na wadau wote wa elimu wameshikamana,  wakaandaa mazingira, wakasimamia, hatimaye Mkoa umeiona njia waliyoitafuta kwa muda mrefu.

Bila mshikamano wa viongozi na wadau wote wa elimu, hata kama kuna fursa nzuri ya kusoma matokeo chanya hayatapatikana. ndiyo maana katika moja ya wimbo wa hayati Bob Marley, ‘Get up Stand up’ anasema.

‘In the Abundant of water, the fool is thirsty’. tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi ni kwamba ‘Katikati ya maji mengi, mpumbavu analia kiu’.

Maneno haya ya Bob Marley ukiyahusianisha na Maneno ya Mheshimiwa Nasha utatambua kwamba wapumbavu hawa anaowataja Bob Marley wanaweza kuwa wameshindwa kuyapata maji kwa sababu ya kukosa uongozi. inawezekana maji haya yako sentimeta tatu ardhini, mhandisi wa maji hajawasaidia. inawezekana maji haya yamefunikwa na majani. inawezekana maji haya yamejazwa kwenye chungu kilichofunikwa, Inawezekana maji haya yanapatikana kwenye miti ya aina fulani. Bila wataalamu na viongozi wao kuwasaidia wataendelea kulia kiu.

Uongozi unahusika katika mafanikio ya jambo lolote.

Sasa tumeianza safari ya mafanikio mkoani Mtwara. Tunapongezana viongozi wote wa mkoa wa Mtwara kwamba tumeweza. Wakati tukifurahia hatua tuliyoifikia tukumbuke maneno ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wakati wa hafla fupi ya kupongezana baada ya matokeo ya kidato cha sita 2018 pale ukumbi wa shule ya sekondari Aquinas.

“Ndugu zangu inaweza isiwe wakati mzuri sana wa kubweteka kwamba tumefanya vizuri. Kuna wasiopenda kuiona Mtwara ikiwa katika nafasi hiyo. hawa watakua na mikakati, watakuwa na mipango, watakuwa na mbinu za kuhakikisha kesho wanaiona Mtwara ikisomeka kumi naa au ishirini”.

Hongereni, Viongozi wa Mkoa wa Mtwara. Mmethubutu na Mmeweza. Mzidi kusonga mbele.No comments:

Post a Comment