MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Saturday, 5 May 2018

Kiwanda cha mbolea Hichoooo Mtwara

Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Phillip Mahiga

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Phillip Mahiga amesema moja ya uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na wajerumani hapa nchini ni ujenzi wa kiwanda cha Mbolea mjini Mtwara. Mheshimiwa Mahiga ameyasema hayo juzi mara baada ya kikao kifupi na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Mhe. Heiko Maas aliyekuwa katika ziara ya siku mbili hapa nchini. Amesema kiwanda hicho kitakuwa kikubwa kuliko vyote Afrika.

 ‘Tumezungumzia eneo la uwekezaji, uwekezaji katika sekta mbalimbali za viwanda. viwanda katika kutengeneza ajira, viwanda kutuwezesha sisi kufikia lengo letu la kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 na Ujerumani kama nchi yenye nguvu, na ambayo ina uwezo mkubwa kuliko nchi zote za magharibi mwa Ulaya inaweza kuwa  Mwekezaji mkubwa katika nchi yetu.
 Tayari sasa hivi tunazungumza uwekezaji wa kiwanda ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote Afrika, kiwanda cha kutengeneza mbolea huko Mtwara. kiwanda ambacho kitasaidia wakulima na kitatengeneza ajira kwa watanzania’ Amesema Balozi Mahiga.

Mheshimiwa Mahiga ambaye anaongoza Wizara ambayo inadhamana ya kujenga mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Nchi za Nje amesema uhusiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria na ndiyo maana Waziri huyo ambaye amepewa nafasi hiyo hivi majuzi ameamua kufanya ziara yake ya kwanza Barani Afrika hapa nchini. Amesisitiza kuwa kutokana na uwezo mkubwa wa uchumi wa taifa la Ujerumani wanauwezo wa kuwa  wawekezaji wakubwa katika nchi yetu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Mhe. Heiko Maas

Majadiliano ya ujenzi wa kiwanda cha mbolea kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya HELM yenye makao yake Ujerumani yalianza miaka kadhaa huko nyuma. Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding) kati ya Kampuni hiyo na Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC) kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Mtwara ilisainiwa Julai 21, 2014.

Mwakilishi wa kampuni ya HELM A.G katika bara la Africa, Mohamed Maatouk.

Matarajio makubwa ya wananchi wa Mtwara ni kuwa kujengwa kwa kiwanda hiki kutawezesha ndoto ya uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuhakikisha ifikapo mwaka 2035 Mtwara kinakuwa kituo muhimu cha uwekezaji na kitovu cha huduma na shughuli muhimu za usafiri na usafirishaji katika ukanda wa mikoa ya kusini mwa Tanzania hususani mikoa ya Lindi, Mtwara Ruvuma na Njombe na ukanda wa maendeleo wa Mtwara ambao unahusisha nchi za Tanzania, Msumbiji, Malawi, Zambia na Afrika ya kusini.

Pia kuifanya Mtwara kuwa Jiji lenye ustawi wa maisha shindani na majiji yaliyo kwenye ukanda wa bahari ya hindi, mashariki na kusini mwa Afrika.

No comments:

Post a Comment