Mpango wa kuhamasisha elimu mkoani Mtwara kwa kuwatambua
walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo umepongezwa na wadau wa
Elimu hapa nchini. Mpango huo ulioanzishwa Na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa
Gelasius Byakanwa unahusisha kuweka vibao vya kumbukumbu ya majina ya Walimu na
wanafunzi waliofanya vizuri kwa kila mwaka.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea maeneo
yanayotekeleza mradi wa Tusome pamoja mkoani Mtwara, iliyofanywa na wadau wa mradi huo kutoka mikoa inayoutekeleza hapa nchini, Mshauri wa
Elimu mkoa wa Lindi kupitia shirika lisilo la kiserikali la ‘Education Quality
Improvement Program’ (EQUIP-T) Digner Peter amesema mpango huo ni mzuri na
unatoa hamasa kwa wanafunzi na walimu kufanya jitihada zaidi.
Digner Peter
“Kilichonifurahisha sana ni vile vibao nilivyoviona hapo shule
ya Msingi Mihambwe. Niliona vibao ambavyo vinamtangaza mwalimu bora na
mwanafunzi bora... Sisi tunaweza kuwa tunakiona kama ni kitu kidogo, Jamani
hicho siyo kitu kidogo kwa wenzetu wazungu wangekikuza hicho. Mtu kuacha
historia nzuri mahari siyo kitu kidogo. Hata kwa hela zangu nitatafuta shule
hata moja Nikakifanye”. Ameeleza Digner.
Kuhusu msaada unaotolewa na Mradi wa Tusome pamoja katika
kuinua elimu mkoani Mtwara Mwalimu Siwema Mrope wa Shule ya Msingi Mbuo Wilayani Mtwara ameshukuru
kwamba hali hiyo imewajengea hamasa watoto kujifunza na kuwaamusha wazazi
kujitolea kuchangia mambo mbalimbali katika elimu.
Siwema Mrope
Amesema yeye binafsi alipatiwa mafunzo ya kufundisha watoto
wadogo. Amesema kabla ya mradi wa tusome pamoja kutekelezwa katika shule yake,
elimu ya awali haikuwa ikipewa kipaumbele. Wazazi na watu mbalimbali katika
jamii walikuwa wakiiona kama vile haina umuhimu. Baada ya kuingia kwa mradi huu
watu wote wametambua na wanatoa ushirikiano wa hali ya juu.
Ameitaka Serikali ihakikishe inawekeza zaidi katika hatua ya
mwanzo ya elimu ya watoto kwani hata maprofesa walijengwa katika hatua ya awali.
Fatuma Mode Ramadhani. Afisa Elimu Maandalizi Zanzibar amesema
amefurahishwa na jinsi ambavyo walimu walivyo na moyo wa kufundisha mkoani
Mtwara. Anasema hali hiyo inaweza isiwe ngeni katika maeneo mengi lakini hiyo
ndiyo njia bora ambayo Taifa linaweza kupiga hatua.
“Lazima kuwepo ushirikiano wa makundi yote hayo katika jamii”.
Alisisitiza.
Rehema Ibrahimu ambaye ni Mhamasishaji Jamii wa shule ya Msingi Mbuo
yeye alisema Mradi wa Tusome Pamoja umeifanya jamii itambue kwamba shule ni
mali yao si mali ya walimu. Jambo lililobaki Tusome pamoja watuwezeshe na sisi
twende tukajifunze kwa wenzetu.
kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Alfred Luanda amewakumbusha
wadau wote wa Elimu kuhakikisha wanazingatia maadili ya elimu. Amesema Taifa bora
litajengwa kwa kuweka misingi imara katika elimu. Ametaja moja ya changamoto
ambazo zinaikumba elimu kuwa ni pamoja na matumizi ya vitabu hasa pale shule zinapotofautiana
katika aina ya vitabu vinavyotumika kufundishia watoto.
Katika ziara hiyo iliyofanywa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mtwara na Tandahimba mkoani Mtwara iliwahusisha wadau kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara,
Morogoro, Iringa na Zanzibar kwa lengo la kujifunza jinsi Mradi wa Tusome
pamoja unaodhaminiwa na Watu wa Marekeni unavyotekelezwa mkoani Mtwara.
Mradi huo umesaidia maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa
walimu jinsi ya kufundisha watoto wa awali na wale wa darasa la kwanza na la
pili. Aidha mradi huu umeenda mbali kwa kuweka miundombinu ya kujifunza na kufundishia
katika shule mbalimbali.
No comments:
Post a Comment