MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Sunday 12 February 2017

Dhahabu ya Kijani yazinduliwa Mtwara. Wananchi waahidi kuchangamukia fursa



Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Seleman Mzee ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi akipanda Mti wa Mkorosho katika shamba la Sallum Namboa wa kijiji cha Dihimba wakati wa uzinduzi wa upandaji miti kimkoa Mtwara.

Uzinduzi wa upandaji miti umefanyika jana mkoani Mtwara huku wananchi wakiahidi kuitumia fursa hiyo kupanda miti aina ya mikorosho maarufu kama "Dhahabu ya Kijani". Zoezi hilo lililofanyika katika kijiji cha Dihimba kilichoko wilayani Mtwara chini ya Usimamizi wa Bodi ya Korosho Tanzania liliwavuta wananchi wengi wa Dihimba ambao walishukuru mkoa kufanya tukio hilo kubwa kijijini kwao.
Mhe. Seleman Mzee akionesha mche wa Mkorosho tayari kumkabidhi Ndugu, Sallum Nachombanga (kulia) wa kijiji cha Dihimba tayari kwa uzinduzi.
 
akizungumza katika uzinduzi huo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Seleman Mzee ameeleza kuwa Korosho inapewa heshima kama dhahabu ya kijani katika mkoa wa Mtwara hivyo jitihada zote zinafanyika ili kuhakikisha inalindwa na kuendelezwa. Amesema mkoa umefanya maandalizi ya kutosha kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la upandaji wa miche 5000 kwa kila kijiji, agizo alilitoa mwishoni mwa mwaka jana akiwa jimboni kwake Luangwa Mkoani Lindi.

Amesema mkoa wa Mtwara una vijiji 792 hivyo kwa miaka mitatu unahitaji miche 3,960,000. Kwa msimu wa 2016/2017 mkoa umeotesha miche 1,248,000 sawa na asilimia 126 ya mahitaji ya mwaka. 

Ametoa wito kwa wanamtwara wote kutekeleza agizo hili kwa kushirikiana na wataalam wa kilimo. Miche yote iliyoooteshwa katika halmashauri zote isambazwe kwa wakulima ili kuwahi majira ya mvua. Aidha Mwisho wa mwezi machi apate majibu ya utekelezaji wa zoezi hili.




Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania Mhe. Anna Abdallah, akizungumza wakati wa uzinduzi. (kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Seleman Mzee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mheshimiwa Anna Abdalla ameagiza vitalu vyote vilivyoko wilayani vianze kazi ili miche yote iingie shambani. Ameeleza kuwa Bodi imejipanga, hivyo mkoa nao utowe ushirikiano ili kuhakikisha zoezi la upandaji mikorosho linafanikiwa. Aidha, mwananchi yeyote asidaiwe fedha kwa ajili ya miche ya mikorosho. Vilevile mikorosho hiyo itolewe kwa wakulima waliofanya maandalizi kadiri ya miongozo ya wataalamu wa kilimo.
Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Korosho Tanzania, Dustan Kaijage (kulia) akikabidhi taarifa  ya hali ya upandaji mikorosho mkoani Mtwara kwa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Seleman Mzee.

Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Korosho Tanzania, Dustan Kaijage ameeleza kuwa wamekamilisha maandalizi ya kupanda mikorosho milioni 30 nchi nzima katika kipindi cha miaka 3.

Ameeleza kuwa Bodi iliingia mkataba na vikundi 60 mkoani Mtwara ili viotesha miche 799,715 ambayo itagawiwa bure kwa wananchi. Upatikanaji wa huduma za ugani, mafunzo mbegu bora na pembejeo limepewa kipaumbele.
Mkulima wa Mikorosho, Sallum Namboa wa kijiji cha Dihimba akishukuru kwa kupewa nafasi ya uzinduzi kufanyika shambani kwake. 

Kwa upande wake Sallum Namboa ambaye zoezi la uzinduzi lilifanyika shambani kwake amesema licha ya miche 90 aliyokusudia kupanda mwaka 2017 amekuwa akijishughulisha na kilimo cha korosho kwa muda mrefu na ameyaona manufaa yake. Ameeleza kuwa katika msimu wa 2016/2017 ambao bei ya kilo moja ya korosho ilipanda hadi shilingi 4000, alivuma tani 7 na kilo 200.

Ameshukuru mkoa kwa kukubali kuzindua upandaji wa miti hiyo katika shamba lake na ameahidi kuhakikisha miche iliyopandwa anaitunza kama alivyoelekezwa na wataalamu.




No comments:

Post a Comment