MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Monday 6 February 2017

Zoezi la uhakiki wa wastaafu laanza kwa mwitikio mkubwa Mkoani Mtwara.



Wahakiki wakiendelea na zoezi katika ukumbi wa Boma Mkoa ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara

Zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa penseni na Wizara ya Fedha na Mipango limenza kwa mwitikio mkubwa huku wastaafu hao wakiitaka serikali kuongeza kiwango cha malipo ya penseni ili kiendani na mahitaji ya sasa ya mabadiliko ya nchi. 
 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Ukumbi wa Boma Mkoa ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara Wakati wa zoezi hilo wastaafu hao wamesema utaratibu wa kutofautisha viwango vya malipo kati ya waliostaafu zamani na sasa hautaisaidia jamii.
Ignasia Ignas Ndunguru, Staff Sajenti Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania akitoa ushauri kwa waandishi wa habari. (hawapo pichani)


Akitolea mfano wa viwango tofauti vya malipo kwa upande wa wastaafu wa jeshi la Wananchi wa Tanzania, Ignasia Ignas Ndunguru, Askari Mstaafu wa jeshi hilo amesema Koplo au Sajenti anayestaafu sasa analipwa kiwango kikubwa kuliko Afisa wa Jeshi Aliyestaaafu miaka 90 Wakati huyo alikuwa na cheo cha juu na pia ndiye alishiriki kwa kiasi kikubwa kuijenga nchi hasa nyakati za ukombozi. Amesema ingependeza kama serikali ingekokotoa mahesabu ya malipo kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya sasa pasipo kutofautisha kama inavyofanyika sasa.

Kwa upande wake Nimrod Kazembe mstaafu wa idara ya Maji Masasi ameitaka serikali iangalie upya mpango wake hasa kutokana na ukweli kwamba Wakati wanaanza kazi mshahara ulikuwa mdogo ukilinganisha na hali ya maisha kwa sasa. Hivyo anaitaka serikali kutozingatia alichokuwa akipata mtumishi kwa wakati ule bali hali halisi ya maisha ya Wakati husika.

Mkaguzi wa Ndani Mkuu Msaidizi wa serikali, Stanslaus Mpembe

Akizungumzia malengo ya uhakiki, Mkaguzi wa Ndani Mkuu Msaidizi wa serikali, Stanslaus Mpembe amesema lengo ni kuiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango kuhuisha taarifa za wastaafu ili kupata kanzi data iliyo sahihi. Pia kuwatambua wastaafu na kuwezesha serikali kulipa wastaafu wanaostahili.

Mpembe amewataka wastaafu wote mkoani Mtwara na Lindi kuhudhulia katika ofisi za Halmsahauri zao kwa ajili ya zoezi hilo ambalo litaendelea kwa siku 5 hadi Februali 10, 2017. Aidha amewataka wastaafu ambao hawana nyaraka zozote kutokana na sababu mbalimbali kufika katika ofisi za Hazina ndogo zilizopo kila mkoa ili waweze kutambuliwa.


No comments:

Post a Comment