MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Wednesday 30 November 2016

Sababu za kusimama uzalishaji Dangote zawekwa wazi


Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwepo na sintofahamu juu ya uzalishaji wa kiwanda cha saruji cha Dangote hasa baada ya saruji ya kiwanda hicho kutoonekana mtaani.

Ili kuondoa minong’ono hiyo, jana Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Halima Dendego aliwaalika Menejimenti ya kiwanda hicho ili kuzungumza na waandishi wa habari juu ya suala hilo. 
Uongozi wa kiwanda hicho uliweka wazi kuwa tatizo kubwa lililosababisha kiwanda hicho kusimama ni masuala ya kiufundi. Hapa nakupa taarifa kamili kwa maneno na video yake ambayo ilisomwa na Meja Mstaafu, Benjamin Kajukano ambaye ni Mkuu wa ulinzi na usalama wa kiwanda hicho.
Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Kiwanda cha Dangote, Meja Mstaafu Benjamini Kajukano akisoma taarifa ya kwa waandishi wa habari (Hawapo Pichani).


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
KUSIMAMA KWA SHUGHULI ZA UZALISHAJI KATIKA KIWANDA CHA DANGOTE MTWARA NOVEMBA 28, 2016.

Uzalishaji katika kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara umeathirika kwa kiasi kikubwa tokea wiki iliyopita. Tatizo hili la muda limetokana na hitilafu ya kiufundi katika mitambo ya Kiwanda. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania Bwana Harpreet Duggal amesema mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea katika siku chache zijazo.

Alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho, jambo lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo. Hata hivyo alizitaja hitilafu hizo kuwa ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi kijacho.

Alipoulizwa kuhusu ngharama kubwa za uzalishaji, Bwana Duggal alisema unapolinganisha na gharama nyingine za uzalishaji katika Dangote, Gharama za uendeshaji Tanzania ni za juu mno. Moja ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizel katika kuendesha kiwanda. Pia kiwanda kuwepo mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la gharama za usafirishaji. Akasema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.

Akaongeza. ‘Tuna matumaini makubwa kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania na tupo makini, kwa kushirikiana na serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili tuweze kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa na bei nafuu nchini’.

Tangu kuzinduliwa kwa kiwanda cha saruji cha Dangote, bei ya saruji nchini Tanzania imeshuka kwa zaidi ya asilimia 30.

Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara chenye thamani ya dola za kimarekani milioni 600 kina uwekezaji mkubwa katika saruji kuliko vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1000 wa Mtwara.


MWISHO
Kiwanda cha Saruji cha Dangote


2 comments:

  1. Lini kitaanza uzalishaji tena wa cement?, maana kikiendelea kusimama gharama za ujenzi wa nyumba zitapanda pia, ni changamoto kwa wawekezaji wetu

    ReplyDelete
  2. Wiki ijayo kitaanza. Hii ni kwa mjibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Harpleet Duggal. Amekuja Ofisini na pia nimemtembelea pale kiwandani.

    ReplyDelete