HUDUMA YA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA
MTOTO
JE! UNAJUA DHUMUNI LA HUDUMA YA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA MTOTO AMBAYO IMEANZA TAREHE 10/12/2019 NA MWISHO TAREHE 10/01/2020?
Mwezi wa Afya na Lishe ya mtoto (Child Health and Nutrition
Month) ni tukio linaloandaliwa na Mkoa kupitia Halmashauri zote ili kutoa
huduma za kinga zilizojumuishwa pamoja na zenye gharama nafuu ili kuboresha
afya na uhai wa mtoto. Tukio hili hufanyika mara mbili kwa kila mwaka, mwezi Juni
na Desemba. Kwa mwezi Desemba 2019, huduma hii imeanza tangu tarehe 10/12/2019
na itafikia tamati tarehe 10/01/2020.
Mkakati huu wa mwezi wa afya na Lishe ya mtoto ni utekelezaji
wa Mpango Mkakati wa Lishe wa Mkoa (Regional
Multisectoral Nutrition Strategic Plan - RMNSP, 2018/19 - 2022/23).
Mpango Mkakati wa Lishe Mkoa
Kuzuia magonjwa yatokanayo na upungufu wa vitamini na madini ni miongoni mwa vipaumbele saba
vilivyopo katika Mpango Mkakati wa lishe wa Mkoa.
Mpango Mkakati wa Lishe wa Mkoa (Mtwara RMNSP) umejikita
kuwekeza katika Lishe haswa kwa kile kipindi cha siku 1000 bora za mtoto (tangu
mimba kutungwa hadi miaka miwili baada ya mtoto kuzaliwa).
Wataalamu wa Sayansi ya Lishe ya Binadamu wanatuambia kuwa
katika kipindi cha siku 1000 ndicho kipindi pekee ambacho ukuaji bora wa ubongo
hufanyika kwa asilimia 90. Aidha, kipindi hiki cha siku 1000 ndicho kipindi cha
kuwapata wataalamu bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
HUDUMA ZINAZOTOLEWA KATIKA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA MTOTO
1. Matone ya Vitamini A hutolewa kwa watoto wote wenye umri kuanzia
miezi 6-59
2. Dawa ya kuzuia minyoo hutolewa kwa
watoto wote wenye umri kuanzia miezi
12-59
3. Tathimini ya hali ya Lishe hufanyika
kwa watoto wote kuanzia miezi 6-59 sambamba na matibabu ya utapiamlo mkali kwa
watoto wote watakao gundulika na matatizo ya kilishe. Matibabu hayo hufanyika
kwa kutumia chakula dawa na maziwa dawa maalumu.
KWA NINI UTOAJI WA MATOENE YA VITAMINI A?
Tatizo la upungufu wa
vitamini A linaathiri takribani asilimia 20% ya watoto ndani ya Mkoa wa Mtwara.
Vitamini A ni muhimu sana katika kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.
Watoto wenye upungufu wa vitamini A wapo katika ongezeko la hatari ya vifo na
maradhi haswa vifo vitokanavyo na surua, maambukizi ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya
kuhara. Upungufu wa vitamini A pia
husababisha tatizo la upofu au kutokuona katika mwanga hafifu.
Vitamini A inahifadhiwa kwenye ini. Dozi inayotolewa kwa
watoto wa miezi 6-59 huweza kuhifadhiwa katika ini kwa miezi 4 - 6. Hii ndiyo
sababu vitamini A hutolewa kila baada ya miezi 6 yaani mwezi wa 6 na mwezi wa
12 kwa kila mwaka
Matone ya vitamini A
Vitamini A huzuia
upofu na kutokuona katika mwanga hafifi.
KWA NINI DAWA YA KUZUIA MINYOO?
Minyoo inapata chakula
kutoka kwenye seli mwilini zikijumuisha seli za damu jambo ambalo husababisha
upungufu wa damu mwilini, udumavu na ukondefu. Aidha, upungufu wa damu huathiri
asilimia 59 ya watoto ndani ya Mkoa. Pia minyoo mviringo inaweza kushindana na
tishu za mwilini katika kupokea Vitamini A katika utumbo. Dawa ya minyoo
inapotolewa kwa watoto huua minyoo ya tumbo na hivyo huwezesha virutubishi
kuimarisha hali ya Lishe ya mtoto.
Dawa ya kuzuia minyoo
KWA NINI KUFANYA TATHIMINI YA HALI YA LISHE ?
Tafiti zinaonesha kwamba
30% ya watoto ndani ya Mkoa wamedumaa wakati 12% wana uzito pungufu na 1.6%
wana ukondefu mkali wakati asilimia 59 ya watoto wana upungufu wa damu. Tathimini
ya hali ya Lishe husaidia kuwagundua mapema watoto wenye matatizo ya kilishe na
kufanya jitihada za haraka ikiwemo matibabu kwa kutumia chakula/maziwa dawa
maalumu.
Tathimini ya hali ya Lishe
Udumavu: kimo kuwa chini
ukilinganisha na umri
Chakula dawa maalumu
Maziwa dawa maalumu
WITO: Wazazi/walezi na jamii kwa
ujumla tutokomeze matatizo ya Kilishe kwa
kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ya mama, baba na mtoto
ili waweze kupata huduma hiyo muhimu.
HUDUMA HIZO
ZINATOLEWA BILA MALIPO.
No comments:
Post a Comment