MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Sunday 28 April 2019

Ulaji unaoshauriwa kwa mgojnwa wa kisukari


Na; Herieth Joseph Kipuyo - Afisa Lishe, Evaristy Masuha-Afisa habari. 
(Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara)

Kwa wasomaji wapya. Hii ni sehemu ya tatu ya makala zinazozungumzia Lishe  ya jamii. Wiki iliyopita tulizungumzia aina za kisukari na namna mgonjwa wa kisukari anavyoweza kudhibiti vyakula vyenye asili ya nafaka, mizizi na ndizi ili visiongeze sukari kwa wingi kwenye damu. Leo tunaendelea kuzungumzia namna mgonjwa wa kisukari anavyoweza kula vyakula kutoka katika makundi mengine ya vyakula.  Tuwe pamoja.

Vyakula asili ya wanyama na vyakula jamii ya kunde. Vyakula jamii ya kunde vina makapimlo kwa wingi (nyuzinyuzi) hivyo mgonjwa wa kisukari anashauriwa kutumia zaidi kama kitoweo na ale tofautitofauti mfano maharage, kunde, njegere, mbaazi, njugu, choroko n.k.  Anashauriwa kupunguza matumizi ya nyama hususani nyama nyekundu na kama italiwa isizidi nusu kilo kwa wiki.  Apendelee zaidi samaki na kuku (kuku aondoe ngozi) ila ale kulingana na mahitaji ya mwili wake kuepuka uzito mkubwa wa mwili.
Vyakula asili ya wanyama na mikunde

Mbogamboga. Mgonjwa anatakiwa kula mbogamboga kwa wingi. Mgonjwa ale mbogamboga tofautitofauti. Mboga za majani zisipikwe bila mafuta kabisa bali zipikwe kwa kiasi kidogo cha mafuta ili virutubishi vyote viweze kufyozwa vyema mwilini. Mbogamboga zikipikwa bila mafuta virutubishi havita weza kufyonzwa mwilini ipasavyo na hivyo mgonjwa anaweza kupata matatizo mengine ya kilishe. Mfano wa mboga mboga ni mchicha, chainizi, matembele, spinachi, kisamvu,  biringanya, bamia, nyanya chungu, kabichi, hoho, n.k. mboga za majani zenye rangi ya kijani ni muhimu kwani ina wingi wa madini ya manganese ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa kichocheo cha insulini.
Mbogamboga

Matunda.  Kula matunda freshi kiasi kidogo kwa kila mlo mfano embe saizi ya kati, chungwa saizi ya kati, ndizi moja ndogo, kipande cha papai, nanasi, tikiti n.k. (tunda usawa wa ngumi moja kwa kila mlo). Kiasi kikubwa cha sukari iliyopo kwenye matunda ni fructose ambayo haihitaji insulini katika kumeng'enywa.  Tumia zaidi matunda kuliko juisi ya matunda na ikiwezekana  tumia matunda na maganda yake bila kumenya mfano. embe, epo n.k. chungwa kula na makapi meupe ya ndani. makapi mlo katika matunda (nyuzinyuzi) husaidia kupunguza kasi ya ufyonzwaji wa sukari mwilini.
Matunda
                        
Vyakula asili ya Sukari, Mafuta na asali. Katika kundi hili epuka sukari na vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, pipi, chokoleti, asali, jamu, biskuti na keki. Mwili huchukua muda mfupi sana kuyeyusha vyakula hivi na hivyo kasi ya kuongeza sukari kwenye damu inakuwa juu. Tumia kiasi kidogo cha mafuta wakati wa kupika na pendelea zaidi mafuta ya mimea kama alizeti, ufuta, nazi, karanga, korosho n.k. Mgonjwa wa kisukari yupo katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo na shinikizo kubwa la damu hivyo aepuke vyakula vyenye mafuta kwa wingi. Mgonjwa asiache kabisa kutumia mafuta.

Vyakula vya asili ya mafuta
Kutokana na aina ya makundi  makuu matano ya vyakula yaliyoainishwa hapo juu, unashauriwa kuchagua chakula kimoja kutoka kila kundi ili uweze kula mlo kamili. Zingatia maelekezo yaliyotolewa katka kila kundi.
KUMBUKA : Mgonjwa wa kisukari hahitaji kula chakula maalumu tofauti na wanafamilia wengine, isipokuwa mlo wake ni lazima uwe na mbogamboga kwa wingi na matunda kwa kiasi kidogo. Pia mlo uwe na nafaka zisizokobolewa kwani ni chanzo kizuri cha makapi mlo (nyuzinyuzi). Makapi mlo yanachukuwa muda mrefu kusagwa tumboni  hivyo kufanya sukari mwilini kutoongezeka haraka.

KUMBUKA : Wewe ni nguzo muhimu katika kumudu ugonjwa huu. Tafuta ushauri wa kitaalamu, usikubali kudanganywa na watu wasiokuwa na uelewa mzuri kuhusu ugonjwa huu. Jiunge na kiliniki ya kisukari ili uendelee kuimarisha Afya yako.

Usikose makala ijayo ambayo itazungumzia mambo ambayo mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuzingatia sambamba na ulaji.


4 comments: