Na, Evaristy Masuha
Vita ya majimaji ilianza Julai 1905 na kumalizika Januari
1907. Pigano la kwanza lilianzia mkoani Lindi katika kijiji cha Nandete wilayani
Kilwa likiongozwa na Mzee wa kimatumbi aliyejulikana kwa jina la Kinjekitile
Ngwale. Miezi miwili baadaye Kinjekitile alikamatwa na Kunyongwa hadi kufa.
Pigano la mwisho lilifanyika katika kijiji cha Lumesule
kilichoko wilayani Nanyumbu mkoa wa Mtwara likiongozwa na kiongozi wa wangindo,
Abdallah Mapanda.
Kijiji hiki kiko katika mpaka wa Wilaya ya Nanyumbu iliyoko
mkoani Mtwara na Wilaya ya Tunduru iliyoko mkoani Ruvuma.
Jambo kubwa linaloitofautisha Lumesule na vijiji vingi
vilivyopigana vita ya majimaji ni kulinda uhalisia ya mazingira ya nyakati za
mapigano ya vita ya majimaji.
Nyakati za vita ya Majimaji sehemu kubwa ya mikoa ya kusini
ilikuwa ni mapori yenye wanyama wakali. Wanyama hao ni moja ya sifa iliyomfanya
mganga maarufu wa kijiji cha Ngalambe huko Kilwa Mzee Kinjekitile Ngwale
kuaminiwa na wananchi wote wa mikoa ya kusini.
Ushahidi huu unapatikana kupitia maandiko ya waandishi mbalimbali
akiwemo John Iliffe kwenye kitabu chake ‘A modern History of Tanganyika’ pamoja
na Fr.
Elzear Ebner katika kitabu chake ‘The History of Wangoni.’ Wawili hawa wanasema Kinjekitile alikuwa na mifugo
mingi ikiwemo Simba na chui. Uwezo wa kufuga wanyama hao pamoja na uwezo wake
wa uganga wa asili ulifanya dunia ya mikoa ya kusini iamini taarifa yake ya
kugundua dawa ya kubadili risasi za Wajerumani kuwa maji kwa kutamka neno la
kimatumbi ‘Mase’ ambalo maana yake kwa Kiswahili ni Maji.
Msitu wa Lukwika-Lumesule
Miaka zaidi ya mia moja baadaye sehemu pekee katika mikoa ya kusini
ambako unaweza kuwaona simba, chui, na wanyama wengine wenye sifa sawa na simba
wa Kinjekitile ni katika msitu wa hifadhi ya kijiji cha Lumesule ambayo
imeungana na kijiji jirani cha Lukwika. (Hifadhi ya wanyama ya Lukwika-Lumesule).
Simba wa Lukwika-Lumesule hawajafugwa lakini ni wapole kama simba wa Kinjekitile.
Pia mita kadhaa kutoka Lumesule unaweza kuuona mlima wa Makong’ondela
ambao una mapango makubwa ambayo ndani yake panaaminika kuwemo mafuvu ya
binadamu. Zipo simulizi nyingi juu ya chanzo cha mafuvu haya lakini Wengi wanayahusisha
na wahanga wa vita ya majimaji ambayo zaidi ya waafrika 75,000 wanatajwa kuuawa
katika maeneo mbalimbali kulikopiganwa vita hii.
Licha ya simba na mafuvu hayo bado yupo nyani muongoza watalii ambaye anapatikana katika mlima wa Mahinyo ulioko kijijini Chivilikiti kilometa kadhaa kutoka Lukwika. Nyani huyu mpole amekuwa kivutio kwa wageni kutokana na ukarimu wake wa kupokea mizigo ya wageni na kuwaongoza katika maeneo mbalimbali ya mapango ya mlima huo.
Licha ya simba na mafuvu hayo bado yupo nyani muongoza watalii ambaye anapatikana katika mlima wa Mahinyo ulioko kijijini Chivilikiti kilometa kadhaa kutoka Lukwika. Nyani huyu mpole amekuwa kivutio kwa wageni kutokana na ukarimu wake wa kupokea mizigo ya wageni na kuwaongoza katika maeneo mbalimbali ya mapango ya mlima huo.

Pamoja na ukweli kwamba sehemu kubwa ya kumbukumbu ya vita ya
Majimaji inapatikana huko Songea bado wageni wanaotembelea kumbukumbu hizo hasa
waliosoma vizuri historia hupata muda wa kutembelea Lumesule kujionea simba wa
Kinjekitile na nyani wa Mahinyo.
Ukiachilia mbali umaarufu wa kihistoria wa kijiji cha
Lumesule ambacho sehemu kubwa ya wakazi wake ni Wamakua, kijiji hiki ni moja ya
vijiji ambavyo ni maarufu katika uzalishaji wa zao la korosho kikiungana na
vijiji vingine vya mkoa wa Mtwara katika uzalishaji wa zao hili muhimu katika uchumi
wa mkoa wa Mtwara.
Nyani muongoza watalii akipata chakula baada ya shughuli ndefu ya kuongoza watalii
Kama walivyo wananchi wengine wa Mkoa wa Mtwara wamakua wa
Nanyumbu pia hutumia kaulimbiu ya ‘Mtwara Kuchele’ wakimaanisha Mtwara
Kumekucha. Kaulimbiu hii hutumika mara nyingi katika kutambulisha maendeleo
waliyoyafikia katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na
kiutamaduni.
Kwa kutambua fursa mbalimbali za utalii zilizoko wilayani Nanyumbu
Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Moses Machali aliyeteuliwa kuongoza Wilaya hiyo
hivi karibuni ameahidi kuifanya Nanyumbu Kuchele kwelikweli. Moja ya mikakati
yake ni kuhakikisha fursa zote za utalii wilayani Nanyumbu zinatambulishwa
duniani kote.
No comments:
Post a Comment