MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Sunday 11 December 2016

Uwezo wa bandari ya Mtwara hadharani. Meli mita 200 yashusha malori ya Dangote



Bandari ya Mtwara imeendelea kuonesha uwezo mkubwa wa kutoa huduma baada ya kupokea meli yenye urefu wa mita 200 sawa na viwanja viwili vya mpira. Meli hiyo iliyoleta malori 651 ya kampuni ya Dangote inayozalisha saruji mkoani hapa ilitia nanga bandari ya Mtwara jana saa 10:30 jioni ikitokea nchi za Mashariki ya Mbali.


Akizungumza baada ya mapokezi ya meli hiyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Dr. Khatib Malimi Kazungu amesema hiyo ni ishara kwa watanzania na dunia nzima kuwa Bandari ya Mtwara ina uwezo mkubwa katika kuhudumia meli za aina yoyote.

Amesema watanzania wanapaswa kuachana na porojo za mtaani ambazo zimekuwa zikiwataka waamini kuwa bandari ya Dar es Salaam ndiyo yenye uwezo tu.

Kwa upande wake Meneja utekelezaji kampuni ya Diamond Shipping iliyosimamia kuja kwa meli hiyo, John Lemomo amesema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba magari 6500 ni ya kisasa kabisa na ina ghoraja 13 ambapo 12 kati yake ni kwa ajili ya kubeba mizigo Wakati ghorofa ya mwisho ni kwa ajili ya huduma ya malazi, chakula na ‘control room’

Amesema pamoja na malori 651 ya Dangote meli hiyo imebeba magari 700 yanayoenda kushushwa Dar es Salaam, na mengine zaidi ya 2000 yanapelekwa Kenya.


Meneja utekelezaji kampuni ya Diamond Shipping Company LTD, John Lemomo, akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani)


Lemomo amesema kabla ya kuamua kuileta meli hiyo hapa Mtwara walijiuliza maswali mengi hasa juu ya uwezo wa bandari hiyo kupokea meli ya aina hiyo. Baada ya mawasilianio na vielelezo vya kitaalamu kutoka pande zote mbili waliamini kuwa inawezekana hivyo wakaamua kufanya hivyo, jambo ambalo kweli limewezekana.



Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda amesema huu ni muda wa wananchi kubadili mtazamo. Kama ilivyozoeleka hapo zamani kuona mizigo ikitoka Dar es salaam kuja Mtwara, leo dunia ikubali mageuzi haya kuwa sasa ni muda wa Dar es Salaam kuiona mizigo ikitokea Mtwara kwenda kwenda huko.
Mapinduzi ya ujio wa viwanda Mtwara inawezekana na mazingira yote ya kuruhusu hali hiyo yameandaliwa. ‘Alisisitiza’



Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda akizungumza na wageni waliokuja kushuhudia tukio.

Wakati meli hiyo ikitua bandarini hapo, shangwe na nderemo zilisikika toka kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara. Akielezea furaha yake, Flora Millinga mkazi wa Mtwara amesema furaha yake imechanganyika na mambo mawili makuu. Kwanza meli hiyo imeidhihirishia dunia kuwa Bandari ya Mtwara ni bora na ina uwezo mkubwa katika kuhudumia meli za aina yoyote.
Aidha tukio hilo pia limezima kelele za watu walioanza kueneza uvumi kuwa Dangote atafunga kiwanda chake na kuhamia Kenya. 

Kutua kwa meli hiyo kumekuja wakati mmiliki wa Kiwanda cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote akiwa ametoa maelezo yenye kusisitiza kuwa ana matumaini na Tanzania. Ana matumaini na kiwanda chake cha Saruji kilichoko hapa Mtwara hivyo hana ndoto tofauti na kuwekeza zaidi nchini Tanzania. 

Maelezo hayo pamoja na tukio la kushusha magari hayo inazima ndoto za sintofahamu iliyotawala kwa muda kadhaa hapa nchini kuwa atakifunga kiwanda hicho.  


 Wananchi wa mkoa wa Mtwara wakiwa eneo la Bandari tayari kushuhudia tukio la Meli yenye malori ya Dangote kutia nanga bandarini hapo.

2 comments: