Walimu Wakuu wa shule za Kidato cha Sita Mkoani Mtwara wakiwa na vyeti vya pongezi walivyokabidhiwa na Mhe. Mkuu wa Mkoa kutokana na kuwezesha mkoa kuwa wa kwanza katika matokeo ya kidato cha sita 2018. waliokaa ni viongozi wa mkoa wa Mtwara wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (wa Nne kutoka kushoto)
Umoja na mshikamano kati ya walimu, wanafunzi, viongozi wa
serikali na wadau mbalimbali wa Elimu umetajwa kuwa sababu kuu ya ufaulu wa
mitihani ya kidato cha sita mkoani Mtwara. Umoja huo umewaimarisha na kuwatia
moyo walimu na wanafunzi katika kutatua changamoto mbalimbali za kielimu hatimaye
kuufanya mkoa wa Mtwara kuwa wa Kwanza katika mitihani ya kidato cha sita
kitaifa mwaka 2018.
Mkuu wa Mkoa akimvalisha Medali Maalumu Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandahimba Moses Mathias shule ambayo imekuwa ya kwanza kimkoa na kushika nafasi ya 27 kitaifa matokeo ya kidato cha Sita 2018
Hayo yamesemwa leo na walimu wa shule mbalimbali za kidato
cha tano na sita mkoani Mtwara wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa kwa lengo la kuwapongeza walimu
hao.
Akifafanua misingi ya umoja huo Mwalimu Hansi Kipamila wa
shule ya sekondari Tandahimba ambayo imekuwa ya kwanza kimkoa na kushika nafasi
ya 27 kitaifa amesema shule imeweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa elimu
ambayo imewezekana kutekelezwa kutokana na umoja na mshikamano.

Mikakati mingine ni motisha kwa walimu na wanafunzi ambayo
hutolewa na Mkuu wa shule pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo jambo ambalo
limeongeza morali ya kufundisha na kujifunza kwa wanafunzi.
Amesema wakati mwingine walimu wa masomo ya pamoja
hushirikiana kuingia madarasani ili kutatua changamoto za wanafunzi kwa pamoja.
Mwalimu Gasper Wechande
Naye mwalimu Gasper Wechande wa shule ya sekondari Kiuta
amesema utaratibu wa kumaliza mitaala mapema umewasaidia kwani hupata muda mrefu
wa kufanya majaribio ambayo husaidia kugundua kasoro za mwanafunzi mmoja mmoja.
Pia huwagawanya wanafunzi wanaopata ufaulu wa chini na wale wanaopata ufaulu wa
juu ambapo wale waliopata ufaulu wa chini hupewa muda wa ziada katika makundi
yenye walimu wa kuwasimamia ili waendane na wenzao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara, Paul Kaji akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa
Aidha mwalimu Mkuu wa Shule ya Ufundi ya Mtwara, Mwl. Paul Kaji ameeleza kuwa njia nyingine ambayo imekuwa
msaada katika kufanikisha matokeo mazuri kwa wanafunzi wa shule yao ni mtihani
maalumu wa kuwajengea kasi ya kumaliza mtihani kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius
Byakanwa amewapa vyeti vya pongezi shule zote zilizofanya vizuri na kuwataka
waendelee na jitihada hizo kupitia kauli mbiu aliyoitambulisha kwa lengo la
kuwataka watokomeze ufaulu wa daraja la sifuri. “Mtwara is a zero free zone in
form six results, Play your part”.
Ameagiza kila shule ihakikishe inalenga wanafunzi kufaulu kwa
daraja la kwanza hadi la tatu. Amesema hilo linawezekana kwani mfano mzuri
umeonekana katika matokeo ya mwaka huu ambapo wanafunzi 1,020 kati ya 1499
wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la pili. Aidha ametoa pongezi maalumu kwa
shule za serikali kuongoza kwa nafasi ya kwanza hadi ya 5 katika mkoa. Amesema
hilo ni jambo la kujivunia kwani hayo ni mageuzi makubwa ya Elimu mkoani.
Awali akisoma matokeo ya ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka 2018
Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara Germana Mung’aho amesema ufaulu wa kidato cha sita
kwa mwaka 2018 Mkoa wa Mtwara umekuwa wa kwanza kati ya mikoa 29 ya Tanzania.
Nafasi hiyo imefikiwa baada ya watahiniwa wote 1499
waliofanya mtihani huo toka Mkoani Mtwara kufaulu kwa asilimia mia. Aidha wanafunzi 11 tu ndio wamefaulu kwa daraja la
Nne huku wengine wote wakiwa wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.
Afisa
Elimu Mkoa wa Mtwara, Germana Mung'aho (Wa sita toka kulia waliosimama)
akiwa pamoja na walimu wa kidato cha tano na sita pamoja na baadhi ya
viongozi wa elimu mkoani Mtwara baada ya walimu hao kukabidhiwa vyeti
vya pongezi.
Mtwara ufundi wako vizuri aithee
ReplyDelete