Na; Herieth Joseph Kipuyo - Afisa Lishe, Evaristy Masuha-Afisa Habari- Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Kwa wasomaji wapya. Hii ni sehemu ya
nne ya makala zinazozungumzia Lishe ya
jamii. Wiki iliyopita tulizungumzia namna mgonjwa wa kisukari anavyoweza kula
vyakula kutoka katika makundi makuu matano ya vyakula bila kusababisha wingi wa sukari kwenye damu. Leo tunaendelea
kuzungumzia mambo ambayo mgonjwa wa kisukari anashauriwa kuzingatia sambamba na
ulaji. Tuwe pamoja.
Epuka
matumizi ya pombe. pombe inatoa nishati lishe kwa wingi hivyo huweza kusababisha ongezeko la
sukari katika damu. (Gm 1 ya pombe
ni sawa na kalori 7 hivyo bia moja ni sawa na kalori 840 ambapo ni sawa na
mkate mdogo wa silesi).
Pendelea maziwa yaliyopunguzwa mafuta (low fat milk) usizidishe mililita 250
kwa siku. Kiasi kikubwa cha sukari iliyopo kwenye maziwa ni lactose ambayo
haihitaji insulini katika kumeng'enywa. Mgonjwa anashauriwa kutumia maziwa kwa
kiasi kidogo kwani ina lehemu (cholesterol)
kwa wingi ambayo huweza kuziba mishipa ya damu na kumsababishia mgonjwa
tatizo lingine la magonjwa ya moyo.
Tumia kiasi kidogo cha chumvi. Chumvi
inapotumiwa kwa wingi humweka mgonjwa katika hatari ya kupata tatizo lingine la
shinikizo kubwa la damu. Matumizi ya chumvi kwa mtu mmoja kwa siku ni gramu 5
(kijiko kidogo cha chai).
Fanya mazoezi ya mwili angalau dakika
30 na kutokwa jasho kila siku. Mazoezi ya mwili husaidia mwili kutumia sukari
kwa ufanisi na hivyo kupunguza kiwango cha sukari katika damu.
Epuka msongo wa mawazo
Epuka unene uliozidi. Tafiti zinaonesha
kuwa unene uliozidi au kupita kiasi husababisha seli za mwili kushindwa
kuitikia mwito wa kichocheo cha insulini kupokea sukari kwa matumizi ya mwili
na hivyo kusababisha sukari kuwepo kwa wingi kwenye damu.
Kunywa maji safi na salama ya kutosha
angalau glasi nane au lita moja na nusu kwa siku.
Epuka matumizi ya sigara.
Iwapo unatumia dawa zingatia maelekezo ya
dawa uliyopatiwa na mtoa huduma za Afya. Usiache kutumia dawa isipokuwa kwa
maelekezo kutoka katika kituo cha kutolea huduma za Afya.
Zingatia maelekezo ya ulaji uliyopewa
na mnasihi wa chakula na lishe.
KUMBUKA : Wewe ni nguzo muhimu katika kumudu
ugonjwa huu. Tafuta ushauri wa kitaalamu, usikubali kudanganywa na watu
wasiokuwa na uelewa mzuri kuhusu ugonjwa huu. Jiunge na kiliniki ya kisukari
ili uendelee kuimarisha Afya yako.
Usikose
makala ijayo ambayo itajibu maswali mbalimbali
kuhusu ulaji wa baadhi ya vyakula kwa wagonjwa wa kisukari.
No comments:
Post a Comment