MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Monday, 6 January 2020

yaliyojiri Mkoani Mtwara mwaka 2019

Tumeuaga mwaka 2019. Yako mengi yaliyojiri katika mwaka huo ambayo yaliiweka Mtwara katika uelekeo mpya wa maendeleo. Kwa uchache sana tunaweza kuyatazama haya.

Mkoa ulifunga mwaka 2018 kwa tamasha kubwa lililotambulishwa kwa jina la ‘Msangamkuu Beach Festival.’ Tamasha hili lililenga kuitangaza fursa ya utalii na uwekezaji kupitia fukwe ya Msangamkuu. Mwitikio wa tukio hilo ulionesha matamanio makubwa ya wananchi wa mkoa wa mtwara kulifanya liwe endelevu.
 Viongozi na wananchi wakifuatilia michezo iliyokuwa ikiendelea wakati wa Tamasha la MsangaMkuu Beach Festival 2018

Mwaka 2018 tamasha hilo lilifanyika kwa siku tatu, mwaka 2019 lilidumu kwa miezi miwili likifanyika siku za wikendi.

Tukio hili pia lilichochea matukio mengine ya kutangaza fursa za utalii katika mkoa wa Mtwara. Tukio lingine la aina hiyo lilifanyika huko Masasi Juni 6-9 likitambulishwa kwa kaulimbiu ya 'Masasi Rock Festival, Tukutane Kileleni.' 
Kilele cha Mlima Mkomaindo ambacho kimetangazwa kuwa fursa mpya ya utalii katika mji wa Masasi
Licha ya kuwakusanya wananchi wengi, Masasi Rock Festival ilihudhuriwa na Msanii wa mziki wa kizazi kipya ambaye asili yake ni Mkoani Mtwara Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tamasha la Masasi Rock Festiva lenye lengo la kutangaza utalii wa mji wa Masasi kupitia mlima Mkomaindo. Kulia kwake ni msanii wa Bongo Fleva Rajab Abdul Maarufu kwa jina la 'Harmonize'
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mwaka 2019 pia unakumbukwa kwa mkoa wa Mtwara kuanza kutumia gesi asilia majumbani. Zoezi la uzinduzi wa tukio hili ulifanywa na Waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani septemba 18.

Uzinduzi wa matumizi ya Gesi asilia majumbani. Awamu ya kwanza ya mradi inalenga kuwafikia wateja 300 ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani

Akizindua mradi huo Mheshimiwa Kalemani alisema awamu ya kwanza ya mradi huo inagharimu takribani Bilioni 3.7 ambazo ni fedha za ndani za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Vilevile alieleza kuwa serikali ya awamu ya Tano iko katika mazungumzo na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA-Mtwara) kwa lengo la kupata eneo ka kusimika miundombinu ili kuwezesha gesi asilia kuanza kutumika katika kuendesha magari.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Matukio mengine yaliyotikisa ni lile la kurudisha kiwanda kilichouzwa kwa shilingi milioni 40 wakati thamani yake halisi iilikuwa ni shilingi milioni 656.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa

Kiwanda hiki kilitokana na umoja wa wakulima, wazalishaji na wabanguaji wa korosho kutoka vijiji vya Chakama, Mpindimbi, Maugura, Chiungutwa, Mwena na Temeke huko Masasi ambao waliunda kampuni ya Masasi High Quality Farmers product (MHQP).
Katika mazingira ya kutatanisha kiwanda hicho kiliuzwa kwa Mzee Saidi Khatau.
Uamuzi wa kukirudisha kiwanda hiki ulifanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa. Aidha Mhe. Byakanwa aliagiza wahusika wote waliolifikisha suala hilo katika mazingira hayo kufikishwa TAKUKURU.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mwezi Oktoba 2019 Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa Mkoani Mtwara na kuacha kumbukumbu nzuri ambayo iliufanya mkoa kuwa miongozi mwa mikoa michache ambayo miradi yake yote ilipita.  Miradi iliyofikiwa na Mwenge ilikuwa 69 ambapo miradi 11 iliwekewa mawe ya msingi, Miradi 12 ilifunguliwa, miradi 11 ilizinduliwa huku miradi 35 ikiwa imeonwa na kukaguliwa.
Ofisi ya Halmashauri ya Mji Newala ni moja ya majengo yaliyotembelewa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019. 

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mwaka 2019 pia unakumbukwa kwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Rais Magufuli aliwasili Mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu iliyoanza Aprili 2 hadi 4.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria upanuzi wa uwanja wa ndege Mtwara April 2, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani hapa
Ziara hiyo ilikuwa na neema nyingi kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara. Licha ya kutoa msamaha kwa wanunuzi haramu wa korosho maarufu kama Kangomba kwa sharti la kukili kufanya kosa, Mhe. Rais aliagiza zabuni ya ujenzi wa barabara kati ya Mnivata hadi Masasi mjini, umbali wa takribani kilometa 150 itangazwe. Vilevile akawataka viongozi wa mkoa wa Mtwara kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wakiwemo wawekezaji katika sekta ya korosho.

Rais Mhe. Dkt. John Magufuli akiwa tayari kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin mjini Mtwara

Akizungumzia uamuzi wa ujenzi wa barabara Mheshimiwa Rais alisema lengo la serikali ni kuhakikisha mkoa wa Mtwara unaunganishwa na nchi jirani ikiwemo Msumbiji na Malawi ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi hizo pamoja na mikoa yote kwenda mataifa mengine.

Alisisitiza kwamba serikali iliamua kuwekeza katika upanuzi wa Bandari ya Mtwara pamoja na uwanja wa Ndege wa Mtwara ili kuwezesha bidhaa na abiria wa ndani na nje ya nchi kuifikia Mtwara kwa urahisi.

Miezi kadhaa baadaye Mheshimiwa Rais alitoa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kusini ambayo ujenzi wake ulikuwa umesimama kwa muda mrefu.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Pia yapo matukio ya kuhuzunisha yaliyotokea. Matukio hayo ni pamoja na lile la Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mikindani Abdul Masamba kupoteza Maisha baada ya kupigwa na radi akiwa darasani.  Tukio hilo lilitokea Machi 5, 2019. 
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Matukio mengine ni ya uvamizi  ambapo raia kumi wa Tanzania  na raia wawili wa Msumbiji waliuawa na watu wasiojulikana huku Watanzania wengine sita wakijeruhiwa vibaya katika kijiji cha Mtole kilichopo upande wa Msumbiji mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Tukio hilo lililotokea Juni 26, 2019.
Novemba 12 watanzania wengine sita wakavamiwa na kuuawa katika kijiji cha Ngongo wilaya ya Tandahimba mpakani na nchi ya Msumbiji na  kujeruhi wengine saba
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea majeruhi waliolazwa katika hospitalin ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, (Hospitali ya Ligula) 
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mwaka 2019 mkoa wa Mtwara ulionesha mvuto kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Miongozi mwa wageni hao ni pamoja na Bwana Carl Rehnberg kutoka Sweden ambaye alipiga hodi ofisi ya Mkuu wa Mkoa Februari 4, 2019 akilenga kuwekeza katika sekta ya korosho.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akiwa na mgeni wake Bwana Carl Rehnberg

Bwana Rehnberg ni mmoja kati ya wageni wengi waliokuja na kuonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya korosho. Kutoka ndani ya nchi mkoa ulitembelewa na aliyekuwa mmiliki wa makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi.
Dkt. Mengi (wa tatu kushoto), akizungumza na Menejimenti ya mkoa na Halmashauri ya wilaya Mtwara mara alipotembelea mkoani hapa kwa lengo la kuangalia fursa ya uwekezaj8i katika sekta ya korosho.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Balozi Celestine Mushy akimpa ufafanuzi Mhe. Einer H. Jensen, Balozi wa Denmark nchini Tanzania wakati wa kutembelea maeneo ya uwekezaji ya Mtepwezi na Msijute wilayani Mtwara.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Sekta ya elimu pia ilipata nguvu kubwa kwa matukio mbalimbali ya wadau kusaidia kutatua changamoto za elimu. Hatua ya kwanza ilianza mwaka 2018 baada ya vyombo vya habari kuripoti juu ya Shule ya Msingi Mitambo ambayo wanafunzi wake walidaiwa kusomea chini ya miti. Hali hiyo iliuamusha uongozi wa mkoa ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kutatua changamoto hiyo.

MKuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akipokea hundi toka kwa Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.  Marie Msellemu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara  Januari 30, 2019
Wadau hao kwa pamoja walitoa michango yao iliyolenga kuboresha shule zote kumi katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara ambazo zililipotiwa wanafunzi wake kusomea chini ya miti.

Baada ya tukio hilo ikaja kampeni ya shule ni choo ambayo iliwakutanisha makundi mbalimbali ya kijamii kuchangia ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari.

Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (MB) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya shule ni choo


No comments:

Post a Comment