MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Tuesday, 7 November 2017

Ulawiti waongezeka Mtwara



Sijawa Omary, Mtwara

VITENDO vya kulawiti watoto wadogo wa kiume kinyume  na maumbile wenye umri wa kuanzia miaka 3 hadi 12 vimekuwa vikiongezeka katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya wakati alipokuwa akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani hapa.

Amesema kuwa, vitendo hivyo kwenye halmashauri hiyo vimekuwa vikiongezeka kuanzia mwezi August hadi Oktoba mwaka huu ambapo jumla ya matukio 11 yameripotiwa kituoni hapo.

Ameyataja maeneo ambayo watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo viovu kuwa ni pamoja na sehemu za mafundisho ya dini, shuleni na majumbani.

Vitendo hivi vinavyoendelea katika jamii zetu ni kinyume na taratibu na ni ukiukwaji wa sheria, lakini pia  kutowatendea haki watoto hawa  ni udharirishaji“,Alisema Mkondya

Ameongeza kuwa kumfanyia mtoto vitendo kama hivyo ni kumsababishia matatizo ya kiafya madhara mbalimbali ya kimwili.
Amesema Jeshi hilo tayari limewafikisha mahakamani watu wawili na linaendelea na uchunguzi wa matukio mengine kadhaa ya aina hiyo.

Hata hivyo Kamanda huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaangalia watoto wao kwa kuwa makini pindi wanaporudi toka maeneo hayo ya dini na shuleni ili kubaini usalama wa mtoto na kuhakikisha hawalali kitanda kimoja na msichana au mvulana  wa kazi (house girl/boy).

“Tatizo linakuja kutokana na wazazi au walezi kupenda kumlaza msichana wa kazi au mvulana wa kazi na mtoto mdogo kitanda kimoja sasa niombe tu jamii au wanamtwara, hii tabia muiache mara moja ili kulinda usalama wa watoto wetu”,Alisema Mkondya.

Vilevile amesema jamii inapaswa kuwandalia mazingira mazuri watoto ili kuondokana na vitendao hivyo viovu vinavyondelea katika halmashauri hiyo ili kulinda usalama wa watoto hao.

Wakazi katika halmashauri hiyo wametoa maoni yao juu ya vitendo hivyo huku baadhi yao  wakilaani wale wote ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kwa watoto hao.

“Maoni yangu mimi kama mkazi wa Mtwara ni kutowafumbia macho wote waliohusika na vitendo hivyo. Lazima sheria ichukuliwe mkondo wake dhidi yao ili iwe mfano kwa wengine”,Alisema Edgar  Mertusi

Veronica Peter ameiomba  mamlaka husika kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaobainika wanafanya vitendo hivyo na kulaani vikali kwani ni moja ya udharirishaji na kutowatendea haki pia ukiukwaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo amesema kuwa, hata katika maandiko ya dini vitendo hivyo vimekuwa vikilaaniwa na kukatazwa. kwani vimekuwa vikimdharirisha mtoto au binadamu na kumfanya ajione hana tena thamani katika jamii sanjali na kumletea athari kubwa kisaikolojia.

Kufuatia hali hiyo jeshi hilo limepanga kufanya operesheni na misako ili kubaini maeneo yote hatarishi ili kuweza kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinaonekana kushamiri hapa mkoani hapa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment