Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Godfrey Uwezo Zambi
amewataka wafanyabiashara wa Korosho kuitumia Bandari ya Mtwara kwani ina uwezo
mkubwa wa kuhudumia shehena hiyo. Amesema hali ya Bandari ya Mtwara kwa sasa ni nzuri hasa baada ya
kutatua changamoto zilizokuwepo mwaka jana. Mheshimiwa Zambi ameyasema hayo jana
mara baada ya ziara yake fupi ya kutembelea bandari hiyo.
Amesema mwaka jana aliwaruhusu wafanyabiashara walionunua
korosho mkoani kwake kufanya uamuzi wao wenyewe iwapo watatumia Bandari ya
Mtwara au Dar es Salaam katika kusafirisha shehena hiyo nje ya nchi kutokana na
malalamiko mengi aliyoyapata kutoka kwa wafanyabiashara wenyewe.
Ametaja baadhi ya changamoto kuwa ilikuwa ni pamoja na uhaba
wa makasha ya kufungia korosho, eneo la kufanyia kazi hiyo na uhaba wa Miundombinu
ya kupakia na kupakua mizigo.
Amesema kwa hali aliyoishuhudia baada ya kutembelea bandari
hiyo hana shaka kuwa changamoto nyingi zimeisha na hivyo Bandari inaweza
kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Ameupongeza uongozi wa Bandari na serikali kwa
ujumla kuamua kufanya jitihada za dhati za kuondoa changamoto hizo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Bandari, Mkuu wa Bandari ya Mtwara,
Nelson Mnali amesema wamejipanga kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati.
Amesema mwaka jana Bandari ilihudumia tani 215,852 ya shehena ya korosho, mwaka
huu wamejiwekea malengo ya kuhudumia tani 230,000 sawa na ongezeko la asilimia 6.5.
Amesema eneo la kuhudumia meli ni kubwa kwa sasa hasa baada
ya kampuni zilizokuwa zimekodi maeneo ndani ya Bandari hiyo kwa ajili ya
kuhudumia kampuni za mafuta ya gesi kumaliza mikataba yao.
Hali hiyo imefanya Bandari iwe na uwezo wa kuhudumia meli
mbili kwa wakati mmoja tofauti na mwaka jana ambapo eneo lilikuwa linawezesha
kuhudumia meli moja kwa wakati. Pia Bandari imewezesha upatikanaji wa makasha ya
kuhifadhia korosho ambapo hadi wakati huo shehena ya makasa zaidi ya 5000 yapo
yakisubiri wateja.
Amewataka Bodi ya Korosho na wafanya bishara kutatua
changamoto zilizoko upande wao ili mizigo ije kwa wingi kwani hali ilivyo sasa uwezo
wa Bandari kuhudumia shehena ni mkubwa kuliko mizigo inayoingia.
No comments:
Post a Comment