ISHI KWA KUFUATA MTINDO BORA WA MAISHA ILI UEPUKE MAGONJWA SUGU YASIYO YA KUAMBUKIZA
Na;
Herieth Joseph Kipuyo, Evaristy Masuha
Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ni kisukari, magonjwa ya
moyo, shinikizo kubwa la damu, magonjwa ya figo, saratani na magonjwa sugu kwa
njia ya hewa.
Kwa Mujibu wa takwimu za Afya Mkoa wa Mtwara (DHIS2, 2018)
watu 34,667 Mkoani Mtwara wameathirika na kisukari, magonjwa ya moyo na
shinikizo kubwa la damu.
Ukiacha takwimu hizi,
Kidunia magonjwa ya saratani, kisukari, matatizo
ya kupumua na maradhi ya moyo husababisha vifo vya watu milioni14 kwa
mwaka ikiwa ni asilimia 71 ya vifo vyote duniani. Idadi hiyo inajumuisha
watu milioni 15 ambao hupoteza maisha mapema kati ya umri wa miaka 30 na 70
kutokana na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza. Hii ni kwa mjibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO, 2018).
Kutokana na ukubwa wa tatizo hili
Afisa Habari Mkoa wa Mtwara, Evaristy Masuha akishirikiana na Afisa Lishe Mkoa,
Herieth Joseph Kipuyo watakuwa wakikuletea mwendelezo wa makala mbalimbali
zinazoelezea njia za kujikinga na maradhi haya sambamba na ulaji unaoshauriwa
kwa mtu aliye athirika na magonjwa tajwa. Makala hizi zitakuwa zikirushwa kila
jumamosi kwenye makundi mbalimblai ya kijamii, tovuti ya Mkoa wa Mtwara www.mtwara.go.tz, mtwarars.blogspot.com, facebook page ya Mtwarars magazeti
pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.
MTINDO BORA
WA MAISHA:
Mtindo bora wa maisha ni ule
unaozingatia ulaji unaofaa, kuepuka matumizi ya pombe, kuepuka uvutaji wa
sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku, kuepuka msongo wa mawazo na kufanya
mazoezi ya mwili.
1. ULAJI UNAOFAA:
Epuka vyakula na vinywaji vyenye sukari kwa wingi. Pendelea
kutumia matunda au juisi halisi ya matunda na mbogamboga kwa wingi. Vyakula
vyenye sukari kwa wingi husababisha uzito mkubwa wa mwili ambao ni miongoni mwa
sababu za magonjwa tajwa hapo juu.
Epuka vyakula vyenye wingi wa
mafuta. Tumia mafuta kidogo wakati wa
kupika na pendelea zaidi mapishi yasiyotumia mafuta mengi kama kuoka,
kuchemsha, kuchoma, mvuke, kutokosa n.k. Halikadhalika epuka vyakula vyenye
lehemu (cholesterol) kwa wingi kama nyama nyekundu ya nguruwe, ng'ombe, mbuzi
n.k. Endapo itatumika mtu mmoja asizidishe nusu kilo kwa wiki. Pendelea zaidi
samaki, nyama ya kuku na vyakula jamii
ya kunde (nyama ya kuku ondoa ngozi). Tumia mafuta ya asili ya mimea mfano
karanga, korosho, alizeti, ufuta, nazi n.k.
Epuka vyakula vilivyopita muda wa matumizi au vyakula
vilivyoharibika/kuoza mfano mahindi, karanga n.k. kwani huwa na sumu kuvu ambayo
huusababisha saratani ya ini.
Epuka matumizi ya chumvi kwa wingi. Matumizi ya chumvi kwa mtu mmoja kwa siku ni gramu 5
(kijiko kidogo cha chai). Chumvi ikizidi huweza kusababisha tatizo la shinikizo
kubwa la damu na baadhi ya saratani kama ya utumbo. Tumia viungo kuongeza ladha
ya chakula badala ya kutumia chumvi kupita kiasi. Viuongo hivyo ni kama
vitunguu saumu, tangawizi n.k.
Kula mbogamboga na matunda kwa wingi punguza wanga na
protini
Epuka unene uliozidi/uliokithiri
Kunywa maji ya kutosha: Maji hayahesabiwi kama kundi la chakula lakini yana
umuhimu mkubwa sana mwilini. Inapaswa kunywa maji safi na salama ya kutosha
angalau glasi nane kwa siku au lita moja na nusu. Unaweza kuongeza maji mwilini
kwa kunywa supu, madafu, togwa na juisi halisi za matunda mbalimbali.
EPUKA MATUMIZI YA POMBE:
Pombe husababisha ongezeko la uzito mkubwa wa mwili
linalohusishwa na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukizwa. Kwa upande mwingine
pombe hupunguza uwezekano wa ini kufanya kazi vizuri na hivyo kuathiri uwekaji
wa akiba ya vitamini na madini mwilini.
Aidha, pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani ya koo,
koromeo, mdomo, matiti n.k.
(Gm
1 ya pombe ni sawa na kalori 7 hivyo bia moja ni sawa na kalori 840 ambapo ni
sawa na mkate mdogo wa silesi).
EPUKA MATUMIZI YA SIGARA NA BIDHAA
NYINGINE ZA TUMBAKU:
Sumu aina ya nikotini iliyopo katika sigara, huharibu ngozi ya ndani ya
mishipa ya damu hivyo huongeza uwezekano wa lehemu (cholesterol) kujikusanya
kwenye mishipa ya damu zilizoathiriwa na kusababisha magonjwa ya moyo. Nikotini
pia huweza kusababisha mishipa ya damu kuziba au kuwa myembamba na hivyo kuzuia damu
kupita inavyotakiwa. Halikadhalika sigara husababisha saratani ya mapafu,
kinywa na koo.
FANYA MAZOEZI YA MWILI :
Ni muhimu kwa binadamu wote, mtoto, mtu mzima mgonjwa au
mwenye afya, mnene au mwembamba kufanya mazoezi kwani husaidia mifumo
mbalimbali ya mwili kufanya kazi kwa ufanisi. Mazoezi huzuia ongezeko la uzito
mkubwa wa mwili, hupunguza uwezekano wa kupata saratani, magonjwa ya moyo na
shinikizo kubwa la damu. Fanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku na
kutokwa jasho. Dumisha mazoezi ya mwili kwa kufanya shughuli mbalimbali za
nyumbani, kutembea kwa miguu badala ya kutumia usafiri wakati wote, kupanda
gorofa kwa ngazi badala ya kutumia lift n.k.
EPUKA MSONGO WA MAWAZO:
KUMBUKA: unene uliozidi au kithiri ni miongoni mwa sababu
inayochangia magonjwa ya kisukari, magonjwa ya moyo na shinikizo kubwa la damu.
Wasiliana na wataalamu ili uweze kujua uzito unao takiwa kuwa nao kulingana na
urefu wako
Tahadhari: Mama mjamzito haruhusiwi
kupunguza uzito hadi atimize miezi sita (6) baada ya kujifungua.
Usikose makala ijayo ambayo itazungumzia ulaji kwa mgonjwa
wa kisukari
Unaweza kupata ushauri au maelezo ya ziada kwa kupiga simu namba 0766269887/0658137610 - Ushauri bure
No comments:
Post a Comment