MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Friday, 10 August 2018

Tatizo la Umeme kwa wawekezaji Mtwara sasa basiMikoa ya Mtwara na Lindi sasa imeandika historia mpya baada ya kuzinduliwa kwa mitambo mipya miwili ya kuzalisha umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati nne na kufanya kituo cha Mtwara kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 22 kutoka megawati 18.
 


Mitambo hiyo imewashwa leo na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani saa 5:20 asubuhi katika kituo cha Mtwara kinachohudumia mikoa ya Lindi na Mtwara. mitambo hiyo imegharimu kiasi cha Sh bilioni 8.5 na hivyo kuongeza wigo mpana katika sekta ya uwekezaji katika miradi inayohitaji umeme.

Akizungumza katika hafla ya kuwasha mitambo hiyo, Dkt Medard Kalemani amesema kutokana na mikoa ya Lindi na Mtwara kukuwa kiuchumi tayari wameanza utaratibu wa kuagiza mitambo mingine miwili ili kufanya kituo cha Mtwara kuzalisha megawati 26 na kuwa na ziada ya umeme lakini kuvutia zaidi wawekezaji hasa wanaohitaji umeme wa uhakika.

  
“Tulichokifanya leo, hizi mashine mbili mpya, tumeziingiza sasa kwenye gridi ya taifa na kuongeza megawati Nne, na kufanya jumla ya megawati 22 kwa mikoa ya Mtwara na Lindi. Kwa sasa mahitaji ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni takribani megawati 16.” Amesema Waziri.
 


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa ameishukuru serikali kwa jitihada wanazoendelea nazo kuhakikisha tatizo la Umeme Mkoani Mtwara linaisha na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuwekeza katika shughuili mbalimbali za kiuchumi ikiwemo viwanda vidogovidogo.
“Sasa umeme wa uhakika upo, ningependa kuona wananchi wanautumia kuboresha maisha yao na hata kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo ili tuweze kufikia katika uchumi wa kati,”amesema Byakanwa
 

Meneja wa mradi Mhandisi, Mkulungwa Chinumba ameishukuru serikali kwa kuhakikisha inatatua changamoto za uzalishaji wa nishati ya umeme mikoa ya kusini. Aidha ameahidi kuzitunza mashine hizo kwa kuweka utaratibu mzuri ya matengenezo pale zinapoharibika.
 
Nao wabunge wa wa mkoa wa Mtwara akiwemo Mhe. Chikota wa jimbo la Nanyamba na Mhe. Hawa Ghasia wa jimbo la Mtwara vijijini wameishukuru serikali kwa kuwezesha kukamilika kwa mradi huo. Wamesema wananchi walikuwa wakikwama kufanya kazi kutokana na kutokuwa na uhakika wa umeme hasa kipindi ambacho mashine zilikuwa zimeharibika.
 
Wamesema msingi wa uchumi wa viwanda ni umeme hivyo wananchi wa mikoa ya Kusini wanapaswa kuchangamkia fursa hii.

Akizungumzia manufaa ya huduma hiyo Yahaya Salumu mkazi wa Mtwara mjini ameishukuru serikali. amesema msingi wa uchumi wa viwanda ni uhakika wa umeme, aidha ameomba gharama za kuingiza umeme majumbani zipunguzwe ili wananchi wengi wa hali ya chini wapate huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment