Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius
Byakanwa ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria Meneja Wa Chama cha
Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU), Afisa Ushirika wilaya ya
Tandahimba, Makatibu wa Vyama kadhaa vya msingi na baadhi ya wananchi
ambao wameshiriki katika ufisadi wa kutisha katika kilimo cha korosho
mkoani hapa.
Mheshimiwa Byakanwa amechukua uamuzi huo
baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa madai ya malipo ya fedha za
wakulima wa korosho msimu wa mwaka 2016/20117 na 2017/2018 katika
Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ambayo iliundwa na Mkuu wa Wilaya
hiyo Mheshimiwa Sebastian Muungano Walyuba.
Amesema katika taarifa hiyo aliyoipokea
wiki iliyopita Wilayani Tandahimba imeonesha Meneja wa Chama Kikuu cha
cha Ushirika cha Wilaya ya Tandahimba na Newala (TANECU) Mohamed Nassoro
alishiriki kufanya maamuzi kinyume na utaratibu hasa baada ya
kubainika upotevu wa kilo 194,479 zilizokuwa zimehifadhiwa katika ghala
lililokuwa chini ya MMZ Company LTD msimu wa 2017/2018. Anasema baada ya
kubainika upotevu huo ambao haukuripotiwa katika chombo chochote cha
ulinzi na usalama viongozi wa TANECU chini ya Meneja huyo walikubaliana
na ahadi ya mtunza ghala huyo kuwa atalipia upotevu huo kwa bei ya tsh
1,850 kwa kilo, ambapo thamani ya kilo zote ni Tsh 359,786,150.
Amesema maamuzi hayo yanatia shaka hasa
ikizingatiwa kuwa bei ya shilingi 1,850 waliyokubalina kulipa kwa kila
kilo ilikuwa ni bei ya chini kabisa katika bei zote kwani korosho
ziliuzwa hadi shilingi 4128. Aidha ameshangazwa na Meneja TANECU
kuchukua uamuzi wa makubaliano hayo wkati uamzi wa nini kifanyike
kutokana upotevu huo ulitakiwa kufanywa na Wakala wa Leseni za Maghala.
Kufuatia hali Hiyo Mheshimiwa Byakanwa ameagiza Meneja wa TANECU
Mohamed Nassoro pamoja na Mwendesha Ghala, Msafiri Zombe akamatwe na
kufikishwa katika vyombo vya dola.
Afisa Ushirika atumbuliwa
Kuhusu usimamizi wa malipo ya wakulima
Mheshimiwa Byakanwa ameagiza Afisa ushirika halmashauri ya Wilaya ya
Tandahimba Sudi Said Rajabu akamatwe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu
kwa kosa la kuruhusu wakulima kulipwa kupitia akaunti binafsi ya Katibu
wa chama cha Msingi cha Upendo ndugu Kazumari Mkadimba kinyume na
utaratibu. Amesema jumla ya shilingi 1,147,465,168/= za wakulima
zililipwa kupitia akaunti binafsi ya Katibu huyo jambo ambalo
linakinznaa na utaratibu wa serikali wa malipo kupitia akaunti ya
mkulima husika. sambamba na hilo Mheshimiwa RC ameagiza kufanya
uchunguzi iwapo wakuilima wamelipwa stahili zao.
Malipo Hewa
Vilevile Mheshimiwa byakanwa ameagiza
kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya msingi waliofanya malipo hewa.
Ameelea kuwa msimu wa mwaka 2016/2017 vyama 12 vilifanya malipo hewa
ambayo thamani yake ni shilingi 117,276,002.00 na hivyo kusababisha
wakulima 156 kukosa malipo. Msimu wa mwaka 2017/2018 tume iligundua
vyama 28 kufanya malipo hewa ambapo jumla ya shilingi 395,783,836.06
zililipwa na hivyo wakulima 328 kukosa malipo. Licha ya viongozi hao na
wanufaika wa malipo hayo kukamatwa ameelekea akaunti zao na zile za
vyama vyao vya msingi kushikiliwa kupisha uchunguzi.
Ucheleweshaji wa malipo
Mheshimiwa Byakanwa amesema uchunguzi wa
Tume, pia umebaini kuwa baadhi ya vyama vya Msingi vilichelewesha
kuwalipa fedha wakulima wa korosho ilihali Chama Kikuu cha Ushirika
TANECU kikiwa kimeingiza fedha husika kwenye vyama vya Msingi. Katika
msimu 2017/2018 uchunguzi umebaini vyama vya msingi 43 vilichelewesha
kuwalipa wakulima 3,343, sawa na kilo 1,286,163 zenye thamani ya Tsh.
3,029,488,791.12 hivyo Mheshimiwa Byakanwa ameagiza malipo hayo
yafanyike mara moja ndani ya wiki mbili na kamati ya Ulinzi na Usalama
Wilaya isimamie suuala hilo.
Kulipa korosho nje ya Mfumo.
Uchunguzi umebaini katika Msimu
2016/2017 na 2017/2018 vyama vya msingi 20 kupitia viongozi wao
wamefanya ubadhirifu na kusababisha kilo 161,869 za Wakulima 624, sawa
na, Tsh 277,521,962.26 kutokulipwa malipo yao. Ameagiza viongozi hao
kukamatwa na akaunti zao kufungwa na kushtakiwa kutokana na ubadhilifu
walioufanya.
Vilevile Mheshimiwa Byakanwa ameagiza benki pia kufanya marekebisho katika utendaji wao kwa kuharakisha malipo ya fedha kwa wakulima. Amesema zipo benki ambazo pia zilichelewesha malipo ikiwemo kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.
Byakanwa amehitisha kwa kuahidi kuwa kwa muda wote atakaokuwa Mtwara hataruhusu mianya ya kunyanyasa wakulima. Kwa yeyote atakayebainika kufanya kinyume na utaratibu atachukua hatua za kisheria. Amewataka wananchi wote wa mkoa wa Mtwara kufuata utaratibu katika utendaji kazi na kujiepusha na mambo yatakayowafanya waingie katika migogoro isiyo ya lazima.
No comments:
Post a Comment