Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa
amemuagiza Katibu Tawala Mkoa, Alfred Luanda kuangalia uwezekano wa kuwahamisha
walimu wa sekondari ili wafundishe shule za Msingi. Mheshimiwa Byakanwa ametoa
agizo hilo wakati wa kikao wa wadau wa Elimu mkoani Mtwara kilichofanyika jana
kwenyeukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida.
Amesema haiwezekani mkoa ukakaa kusubiri Wizara ilete walimu
wakati walimu wapo. Kinachotakiwa ni kufuata utaratibu na kuangalia walio na
sifa za kufundisha shule za Msingi waende bila kuathili mishara yao.
Ametoa agizo hilo kufuatia taarifa ya Afisa Elimu Mkoa Fatuma
Kilimia ambayo ilionesha ziada ya walimu 608 wa masomo ya sanaa kwa shule za
sekondari Mkoani hapa wakati shule za Msingi Mkoani hapa zikiwa na upungufu wa Walimu
2,836.
Katika
taarifa hiyo Kilimia alieleza kuwa mahitaji ya walimu wa masomo ya sanaa kwa
shule za sekondari Mkoani Mtwara ni 1490 waliopo 2098 hivyo kufanya ziada ya
walimu 608.
Wakichangia katika kikao hicho kilichokusudia kuangazia
changamoto za elimu kwa mkoa wa Mtwara wadau wameitaka serikali kuhakikisha
inapambana na masuala mbalimbali yanayozuia maendeleo ya elimu.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Nanyamba Mheshimiwa Abdalah
Chikota ameitaka serikali ihakikishe inafuatilia mwenendo wa elimu kuanzia
ngazi ya shule ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake na
wanaobainika kutotimiza wajibu wao wawajibishwe. Pia ameitaka serikali
kuhakikisha mfuko wa elimu kwa kila halmashauri unasimamiwa ili utumike kwa
lengo lililokusudiwa.
Aidha Mkuu wa Shule ya sekondari Mitengo Mwalimu Amina Bakari
ameitaka serikali iweke viwango ambavyo kila atakayeshindwa kuvifikia atawajibishwa.
Akiridhia wazo hilo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameagiza kila
shule kuhakikisha zinakamilisha mtaala wa darasa husika mwezi wa sita wa kila
mwaka ili muda unaobaki utumike kufanya majaribio na marudio ya vipengele
mbalimbali ndani ya masomo husika.
Mkoa wa Mtwara umekuwa haufanyi vizuri katika mitihani
mbalimbalia ya kitaifa hali ambayo inamfanya Mkuu wa Mkoa Mhe. Byakanwa
aliyechaguliwa kuongoza mkoa huu hivi karibuni kuitisha kikao hicho chenye
lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo. Katika matokeo ya darasa la saba
mwaka jana mkoa ulishika nafasi ya 22 kati ya mikoa 26.
No comments:
Post a Comment