MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Tuesday 23 August 2016

Mtwara yashinda wanasayansi bora Tanzania

Ikiwa ni wiki kadhaa zimepita tangu shule ya Sekondari Tandahimba iliyoko Mkoani Mtwara kutangazwa mshindi katika nafasi kumi bora mtihani wa kidato cha Sita 2016, Shule ya Sekondari ya wasichana Mtwara imeshinda nafasi ya kwanza katika mashindano ya wanasayansi vijana wa Tanzania.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki hii yakiwashirikisha washiliki 150 kutoka shule mbalimbali nchini, wanafunzi Diana Sosoka na Nadhra Mresa wametangazwa washindi kupitia mashine ya kuangua mayai waliyoitengeneza kwa gharama ya shilingi 25,000/=.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kupokelewa uwanja wa ndege Mtwara, Sosoka amesema walisukumwa na wazo la kutengeneza mashine hiyo kufuatia ugumu wa maisha unaowakumba akina mama wengi Mkoani Mtwara na Tanzania kwa ujumla huku wakiwa na rasilimali mbadala ya kuwakomboa.

‘Tulijiuliza njia gani rahisi ambayo akina mama hawa wanaweza kuimudu katika kujikwamua. Tukajiuliza juu ya ufugaji wa kuku ambapo mashinne ya kuangua mayai zimekuwa zikuzwa gharama kubwa ambayo watanzania wengi wakiwemo akina mama wa Mtwara hawaimudu, ndipo tukaja na wazo hili ambalo linawezekana kwa gharama ndogo kabisa’. Anaeleza Diana.

‘Tumetumia vifaa vya kawaida vya mabaki ya mabomba yanayopatikana kwa wajenzi wa nyumba, maboksi na taa ya chemli ya kawaida ambayo kila Mama anaweza kupata’.

Anasema mara ya kwanza wakiwa hapa Mtwara walitengeneza na kuiwasilisha katika mashindano yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Aquinas Mkoani Mtwara mwanzoni mwa mwezi Julai 2016 wakawa washindi wa pili. Baada ya hapo waliendelea kuiboresha na kuitumia katika maonesho ya Nanenane Lindi kisha kuisafirisha kwenda Dar es Salaam tayari katika mashindano yaliyowapa ushindi.

Mchakato wa kumpata mshindi
Akizungumzia mchakato wa kumpata mshindi, Nadhra anasema ilikuwa ni mpambano mkali uliowaacha na hofu kubwa katika kipindi chote cha kuelekea kutangazwa mshindi kutokana na ubora wa vifaa vya wanasayansi wengine, pia wingi wa washiriki.

Amesema washiriki walikuwa 150 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo walichaguliwa washindi katika nafasi mbalimbali za sayansi ya jamii, sayansi ya viumbe hai, sayansi ya kilimo N.K. baada ya kutangazwa nafasi zote walipoteza matumaini kabla ya kutangazwa mshindi wa jumla hali iliyowatoa machozi kwa furaha.

‘Kwa ujumla katika kipindi chote tulikuwa katika wakati mgumu hasa huyu mwenzangu (Diana Sosoka) ambaye alikuwa hawezi hata kutemblea. Tunashukuru tumewawakilisha vema. Tunaamini tutasonga mbele zaidi katika kuendeleza tuliyoyaanzisha ili kuipeleka nchi yetu katika sayansi ya viwanda. Tumeitangaza Mtwara na tutaendelea kuitangaza zaidi. Yote ni kwa mapenzi ya Mungu. Tunashukuru sana’ Anasema Nadhra.

Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego ambaye aliwaalika rasmi ofisini kwake na kuwatambuilisha kwa wadau wa Korosho waliokuwa katika kikao cha kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kilimo cha korosho aliwawakabidhi mchango wa wajumbe wa kikao shilingi 695,000.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amepongeza jitihada za mabinti hao pamoja na walimu wao na kuahidi kuendeleza jitihada walizozifanya. Ameeleza kuwa mkoa unatarajia kuwa na ugeni wa Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Hassan hivyo atatumia nafasi hiyo kuwatambulisha washindi hao kwa mgeni rasmi.

Aidha, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameagiza uongozi wa SIDO kuichukua teknolojia hiyo na kuiingiza katika maabara ya uchunguzi zaidi ili mashine hizo zitengenezwe na zipewe heshima ya kutambuliwa kwa majina ya wavumbuzi hao.

Afisa Elimu Mkoa
Afisa Elimu Mkoa, Fatuma Kilimia amepongeza jitihada hizo na kuwataka wanafunzi na walimu wengine kuiga mfano huo. Ameeleza kuwa huo utakuwa ni mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio. Amewataka washindi hao kutobweteka kwa mafanikio waliyoyapata kwani safari ya mafanikio bado ni ndefu.

Vilevile amewataka kujiepusha na vishawishi ambavyo vinaweza kuwaondoa katika jitihada walizozianzisha.

Mashindano ya wanasayansi vijana yanaendeshwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya ‘Young Scientists Tanzania’ chini ya Udhamini wa British Gas (BG) Tanzania.

Katika mashindano haya washindi hawa wamezawadiwa pesa tasilimu shilingi 1,800,000, safari ya kutembelea Ireland mwezi Januari 2017 na udhamini wa masomo ya chuo kikuu mara watakapomaliza kidato cha sita.

No comments:

Post a Comment