MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Friday, 6 July 2018

Panya choma ‘festival’ yaja Mtwara.


Umaarufu wa mkoa wa Mtwara katika kula nyama ya panya ni fursa mojawapo ya kuvutia utalii mkoani hapa.  Hilo litawezekana iwapo jamii ya watu wanaotumia chakula hicho watawekewa mazingira mazuri ya kujitangaza na kukitangaza chakula hicho kupitia matukio mbalimbali ikiwemo ‘Panya festival’ au panya Choma.

Akizungumza katika kipindi cha safiri nasi kilichokuwa kikirushwa moja kwa moja kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara leo, Mhe. Gelasius Byakanwa amesema hilo ni mojawapo ya malengo yake kuhakikisha fursa mbalimbali za mkoa wa Mtwara ikiwemo ulaji wa nyama ya panya unatumika kama kivutio. Aidha katika ratiba yake amepanga kabla ya mwezi wa saba mwaka huu kuandaa tukio ambalo na yeye atashiriki kula nyama hiyo.  

Anasema fursa hiyo inaweza kuwavuta watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi na kuufanya mkoa wa Mtwara kujulikana zaidi. Aidha itatoa fursa ya kufanya maboresho katika chakula hicho katika mtindo bora na wa kisasa zaidi. 

“Kwa nini tusitangaze, isiwe rasmi kwamba panya ni chakula, tukawakaribisha mikoa mingine kwamba njooni Mtwara tule panya. Lakini kama sisi wenyewe tukikitambua na kukihalalisha kuwa hiki ni chakula bila kuitenga ile jamii… so long as hakina madhara kwa afya ya mtu, na pengine imani yako haizuii, mimi sioni sababu kwa nini tusikichukuwe na chenyewe kikawa kivutio”. Amesema Mhe.Byakanwa.

Mhe. Byakanwa ambaye ni Mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ametolea mfano mkoa huo kwamba ni maarufu kwa ulaji wa Senene na kwamba chakula hicho sasa kimevuka mipaka kutoka Bukoba hadi nje ya nchi.

“Kule Bukoba tunakula senene, mwanzoni senene walionekana wanaliwa Bukoba tu lakini sasa kila sehemu wanakula, mpaka wengine wanakuwa exported nje ya nchi. Kwa nini panya nao wasiwe hivyo? 

Nyama ya panya ni chakula maarufu mkoani Mtwara huku wilaya ya Masasi ikitajwa kuongoza katika ulaji wa nyama hiyo.

No comments:

Post a Comment