Katibu Tawala Mkoa wa
Mtwara Alfred Luanda amewataka Maafisa Utumishi kubuni njia nzuri itakayotoa
motisha kwa watumishi ili kuwafanya wawe na moyo wa kufanya kazi ndani ya mkoa.
Amesema anatambua ugumu wa mazingira na huduma katika baadhi ya maeneo ndani ya
mkoa lakini mipango mizuri yenye kutoa motisha kwa watumishi itawafanya watumishi
waendelee kuwa na moyo wa kufanya kazi katika maeneo waliyopangiwa.
Luanda ameyasema hayo
leo wakati akifungua Warsha ya kuandaa mipango ya motisha ya watumishi wa
serikali za mitaa iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maafisa Tabibu Mtwara
(COTC)
Katika warsha hiyo
iliyoandaliwa na shirika la Watu wa Marekani (USAID) kupitia mradi wake wa PS3
amesema jambo kubwa ni halmashauri zenyewe kujiangalia ili yale ambayo wanauwezo
nayo yapewe kipaumbele katika utekelezaji.
‘Ni kweli kuwa
utekelezaji wa baadhi ya mambo unahitaji fedha nyingi mfano, ujenzi wa
barabara, ujenzi wa nyumba za watumishi, miundombinu ya mawasiliano na mengine
mengi. Haya Serikali itaendelea kuyashughulikia kwa kadiri inavyopata uwezo wa
kutekeleza’.
Amesisitiza kuwa utoaji
wa motisha kwa watumishi utakuwa na maana tu kama utakuwa endelevu hivyo ni
vema mipango ikajengwa ndani ya mifumo ya utendaji wa Halmashauri, ili iwe
rasmi, endelevu na kuingizwa katika mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji.
Kwa upande wake Msimamizi
idara ya Rasilimali Watu Kanda ya Kusini, Mradi wa PS3, Restituta Evaristy
Masau amesema wazo la motisha kwa watumishi wa serikali za mitaa limekuja
kufuatia utafiti uliofanywa na shirika lao wakipitia sera ya motisha kwa
wafanyakazi na kubaini kuwa ni ngumu kuitekeleza.
Kufuatia utafiti huo
ndipo shirika likaona umuhimu wa kuwapa mafunzo Maafisa wa Halmashauri ili
waweze kuandaa mpango unaotekelezeka. Anasema mradi huo wa PS3 unaodhaminiwa na
watu wa marekani una nia ya kuhakikisha watanzania wanaondokana na changamoto
wanazokutana nazo katika mazingira ya kazi, hivyo kuachana na tabia ya kuhama
hama kituo kimoja kwenda kingine kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Warsha, Tamko Mohamed Alli ambaye pia ni Afisa Utumishi Manispaa ya Mtwara
Mikindani anasema ziko changamoto nyingi katika halmashauri za mkoa wa Mtwara ambazo
zinawafanya watumishi kupenda kufanya kazi eneo moja na kuchukia maeneo
mengine. Anasema kubwa linalowavutia ni miundombinu ya eneo husika hivyo warsha
hiyo itakayoendeshwa kwa siku tano itasaidia kwa kiasi kikubwa kupata mpango
mpya wa motosisha kwa wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment