TANGAZO la Septemba 23, 2016 kwenye gazeti la HabariLeo
liliwataka Watanzania hususan wanaMtwara kujitokeza kutoa maoni yao
dhidi ya Mpango Kabambe wa Mji wa Mtwara ambao uko katika hatua za
mwisho kupitishwa. Jumapili ya Oktoba 10, 2016 Katibu Tawala wa Mkoa
huo, Alfred Luanda ambaye pia ana taaluma ya mipangomiji aliwatangazia
wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara siri iliyoko ndani ya
mpango huo.
Luanda alisema mpango huo unajibu hoja zote za jinsi
mji wa Mtwara utakavyosimamiwa kwa miaka 20 ijayo. Mpango umehusisha
eneo lote la Manispaa ya Mtwara Mikindani na kata tisa za Halmashauri ya
wilaya ya Mtwara.
Siku hiyo hiyo, kabla ya tangazo la Mpango
Kabambe, Kamati ya Ushauri iliridhia ombi la Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Beatrice Dominic la kuifanya Manispaa
hiyo kuwa Jiji. Tafsiri nyepesi ni kuwa wote walioshiriki katika maamuzi
haya wana matumaini makubwa na mwenendo wa mkoa katika kukua na
kuimarika katika nyanja nyingi za maendeleo.
Kutokana na ukweli
kuwa viwanda ni hatua mojawapo ya kuufanya mji kukua, makala haya
yanaangazia Mtwara katika azma ya kuelekea mji wa viwanda.
Hali ya sasa viwanda Mtwara.
Ukweli
unaoonekana wazi ni kuwa enzi za watumishi kujuta pale wanapopangiwa
Mtwara zinaendelea kubaki historia na badala yake sasa watumishi
watapigania kupangiwa Mtwara. Mtwara ya sasa ina mvuto mkubwa kwa
wawekezaji hasa kutokana na kuonesha uelekeo wa kutatua changamoto ya
umeme.
Viwanda vikubwa vilivyopo na ambavyo vinajulikana sana kwa
sasa vipo vinane. Viwanda hivyo vitano ni vya kubangua korosho, kimoja
cha kuchakata gesi asilia pamoja na viwili vya saruji kikiwemo kiwanda
cha Dangote ambacho ni kikubwa kuliko vyote katika Ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati.
Akizungumza na wamiliki wa nyumba za kulala
wageni zilizoko Mtwara mjini mapema mwezi huu, Mkuu wa Mkoa, Halima
Dendego aliwahakikishia kuwa mkoa umeweka mazingira mazuri ya kuvutia na
kuruhusu uwekezaji na kwamba amekuwa akipokea wageni wengi. Miongoni
mwa wageni hao anasema ni pamoja na wale wanaohitaji kuwekeza katika
sekta ya viwanda.
Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu viashiria vya
Mtwara ya viwanda viliendelea kujionesha baada ya Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa kukata kiu ya sintofahamu
ya muda mrefu ya wakazi wa Mtwara ya kutaka kujua iliko ahadi ya ujenzi
wa kiwanda kikubwa cha mbolea cha HELM.
Ntalikwa aliwaeleza
wanaMtwara kuwa kiwanda kilichelewa kutokana na hofu ya uwepo wa gesi
asilia ya kutosha na kwamba sasa upo uhakika usioacha chembe kwamba
rasilimali hiyo ipo ya kutosha kuwezesha kiwanda hicho kujengwa.
Alieleza
kuwa mahitaji ya kiwanda hicho ni futi za ujazo trilioni 0.8 wakati
vituo vya Ntorya na Msimbati vyote vya Mtwara vina uwezo wa kuzalisha
futi za ujazo trilioni 2.05, hivyo ni wazi kuwa kiwanda cha HELM
kinakuja katika eneo la MsangaMkuu mkoani hapa.
Kwa nini viwanda havikwepeki mkoani Mtwara?
Mambo
makubwa yanayoipeleka Mtwara kuwa eneo la Viwanda ni uwepo wa umeme wa
kutosha na wa uhakika unaotokana na ugunduzi wa gesi asilia na mipango
ya mapema ya kuupanga Mji wa Mtwara kupitia Mpango Kabambe wa mji huo.
Mengine
ni jiografia na historia ya mkoa. Kwa sasa wengi wanaoiangalia Mtwara
kwa kuitofautisha na mikoa mingi ya nchi hii ikiwemo Dar es Salaam ni
kukamilika kwa wakati kwa Mpango Kabambe wa mji huo. Hii ndiyo njia moja
kubwa anayoiamini mwekezaji kuwa itamuepusha na migogoro ya ardhi.
Mpango
huu unakuja wakati mkoa haujaingia katika ujenzi holela kama ilivyo
mikoa mingine hapa nchini. Mtwara ni mji ambao unafananishwa na mji wa
Tanga kwa kupangika sawasawa. Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipotembelea
mkoa wa Mtwara wakati wa ufunguzi wa Kiwanda cha Dangote na kile cha
kuchakata gesi asilia cha Madimba aliusifia mji kwa kuwa na mpangilio
mzuri.
Hili limewezekana kutokana na historia ya mkoa kuwa
ulipimwa na wakoloni, kisha ukasimama kuendelea kutokana na sababu za
kihistoria hasa mapambano ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
Barabara
za Mtwara zimepangika vizuri na pana kiasi kwamba upanuzi wa mji
hautahitaji kubomoa nyumba. Hiyo ni ziada ya matumaini ya kuiona Mtwara
ya maendeleo ya viwanda ikiendelea kuwa na mwonekano mzuri. Licha ya
sifa ya kuwa na Mpango Kabambe wa Mji, mkoa unayo ardhi ya kutosha kwa
kilimo na shughuli nyingine za uwekezaji.
Hii imekuwa ikichangia
mkoa kuongoza kwa asilimia 75 ya uzalishaji wa korosho nchini Tanzania.
Zao hili pia ni mvuto kwa wawekezaji wa viwanda vya kubangua korosho.
Andiko
la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, ‘Opportunity for Investment’
linalopatikana katika http://www.mtwara.go.tz/pages/the-
opportunities-for- investment linaonesha kwamba mkoa wa Mtwara wenye
eneo la kilometa za mraba 16,720 unazo hekta 1,400,00 zinazofaa kwa
kilimo.
Dendego anafafanua kuwa eneo hilo lina rutuba ya kutosha na halijatumiwa ipasavyo hivyo anaalika wawekezaji kulitumia.
Kwenye
barua ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Mtwara Mikindani
kuwashawishi wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa kuifanya Mtwara kuwa
jiji anataja baadhi ya mambo ambayo yanaonesha kuwa mkoa huo ni
endelevu.
Anasema Mji wa Mtwara ndio kitovu cha uchumi wa mikoa
ya kusini mwa Tanzania ikiwemo Lindi na Ruvuma. Mkoa huu kwa sasa
unajengwa Tawi la Benki Kuu ambalo kwa mujibu wa Rais mstaafu Kikwete
wakati akiwaaga wakazi wa Mtwara, tawi hilo limekuja kutokana na
viashiria vya kukua kwa haraka kwa mji huo.
Kikwete ambaye mpango
wa ujenzi huo ulianza katika kipindi chake cha uongozi anasema anaiona
Mtwara itakayokuja kuwa mhimili wa uchumi wa nchi hii. Ujenzi wa reli
itakayosaidia kusafirisha makaa ya mawe toka Liganga na Mchuchuma uko
katika hatua nzuri.
Upanuzi wa Bandari ya Mtwara ikiwemo mpya ya
Kisiwa Mgao iliyoko katika mipango ya ujenzi ni viashiria vipya vya
mvuto kwa uwekezaji wa viwanda.
Barabara nzuri, bandari, reli, na
uwanja wa ndege vyote vinapatikana mkoani Mtwara, mambo ambayo
yanaonesha kuwa Mtwara ni ya viwanda inawezekana.
No comments:
Post a Comment