MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Tuesday 31 December 2019


HUDUMA YA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA MTOTO

JE! UNAJUA DHUMUNI LA HUDUMA YA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA MTOTO  AMBAYO IMEANZA TAREHE 10/12/2019  NA MWISHO TAREHE  10/01/2020?

Mwezi wa Afya na Lishe ya mtoto (Child Health and Nutrition Month) ni tukio linaloandaliwa na Mkoa kupitia Halmashauri zote ili kutoa huduma za kinga zilizojumuishwa pamoja na zenye gharama nafuu ili kuboresha afya na uhai wa mtoto. Tukio hili hufanyika mara mbili kwa kila mwaka, mwezi Juni na Desemba. Kwa mwezi Desemba 2019, huduma hii imeanza tangu tarehe 10/12/2019 na itafikia tamati tarehe 10/01/2020.
Mkakati huu wa mwezi wa afya na Lishe ya mtoto ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Lishe wa Mkoa (Regional Multisectoral Nutrition Strategic Plan - RMNSP, 2018/19 - 2022/23).

Mpango Mkakati wa Lishe Mkoa
        

Kuzuia magonjwa yatokanayo na upungufu wa vitamini na madini ni miongoni mwa vipaumbele saba vilivyopo katika Mpango Mkakati wa lishe wa Mkoa.
Mpango Mkakati wa Lishe wa Mkoa (Mtwara RMNSP) umejikita kuwekeza katika Lishe haswa kwa kile kipindi cha siku 1000 bora za mtoto (tangu mimba kutungwa hadi miaka miwili baada ya mtoto kuzaliwa).
Wataalamu wa Sayansi ya Lishe ya Binadamu wanatuambia kuwa katika kipindi cha siku 1000 ndicho kipindi pekee ambacho ukuaji bora wa ubongo hufanyika kwa asilimia 90. Aidha, kipindi hiki cha siku 1000 ndicho kipindi cha kuwapata wataalamu bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

HUDUMA ZINAZOTOLEWA KATIKA MWEZI WA AFYA NA LISHE YA MTOTO
1.     Matone ya Vitamini A  hutolewa kwa watoto wote wenye umri kuanzia miezi 6-59
2.     Dawa ya kuzuia minyoo hutolewa kwa watoto wote wenye umri  kuanzia miezi 12-59
3.     Tathimini ya hali ya Lishe hufanyika kwa watoto wote kuanzia miezi 6-59 sambamba na matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wote watakao gundulika na matatizo ya kilishe. Matibabu hayo hufanyika kwa kutumia chakula dawa na maziwa dawa maalumu.

KWA NINI UTOAJI WA MATOENE YA VITAMINI A?
Tatizo la upungufu wa vitamini A linaathiri takribani asilimia 20% ya watoto ndani ya Mkoa wa Mtwara. Vitamini A ni muhimu sana katika kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. Watoto wenye upungufu wa vitamini A wapo katika ongezeko la hatari ya vifo na maradhi haswa vifo vitokanavyo na surua,  maambukizi ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya kuhara. Upungufu wa vitamini A pia husababisha tatizo la upofu au kutokuona katika mwanga hafifu.
Vitamini A inahifadhiwa kwenye ini. Dozi inayotolewa kwa watoto wa miezi 6-59 huweza kuhifadhiwa katika ini kwa miezi 4 - 6. Hii ndiyo sababu vitamini A hutolewa kila baada ya miezi 6 yaani mwezi wa 6 na mwezi wa 12 kwa kila mwaka

Matone ya vitamini A


Vitamini A huzuia upofu na kutokuona katika mwanga hafifi.


KWA NINI DAWA YA KUZUIA MINYOO?
Minyoo inapata chakula kutoka kwenye seli mwilini zikijumuisha seli za damu jambo ambalo husababisha upungufu wa damu mwilini, udumavu na ukondefu. Aidha, upungufu wa damu huathiri asilimia 59 ya watoto ndani ya Mkoa. Pia minyoo mviringo inaweza kushindana na tishu za mwilini katika kupokea Vitamini A katika utumbo. Dawa ya minyoo inapotolewa kwa watoto huua minyoo ya tumbo na hivyo huwezesha virutubishi kuimarisha hali ya Lishe ya mtoto.

Dawa ya kuzuia minyoo


KWA NINI KUFANYA TATHIMINI YA HALI YA LISHE ?
Tafiti zinaonesha kwamba 30% ya watoto ndani ya Mkoa wamedumaa wakati 12% wana uzito pungufu na 1.6% wana ukondefu mkali wakati asilimia 59 ya watoto wana upungufu wa damu. Tathimini ya hali ya Lishe husaidia kuwagundua mapema watoto wenye matatizo ya kilishe na kufanya jitihada za haraka ikiwemo matibabu kwa kutumia chakula/maziwa dawa maalumu.

Tathimini ya hali ya Lishe


Udumavu: kimo kuwa chini ukilinganisha na umri                                                                                               

Chakula dawa maalumu 



                 Maziwa dawa maalumu


WITO: Wazazi/walezi na jamii kwa ujumla tutokomeze matatizo ya Kilishe kwa  kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ya mama, baba na mtoto ili waweze kupata huduma hiyo muhimu.

HUDUMA HIZO ZINATOLEWA  BILA MALIPO.







No comments:

Post a Comment