MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Thursday 20 June 2019



Timu ya Mpira wa wavu (Volleyball) ya wasichana ya Mkoa wa Mtwara ambayo inashiriki katika mashindano ya UMISETA  mwaka 2019 imechukua ubingwa wa mashindano hayo baada ya kuwashinda timu ya Mkoa wa Dar es Salaam seti 3-0. Mashindano haya yanayofanyika kitaifa mkoani Mtwara yalifunguliwa rasmi Juni 10, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) na yanatarajiwa kufungwa kesho Juni 21 na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.
Mgeni Rasmi ambaye pia ni katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Dkt. Jilly Maleko akizungumza na wachezaji kabla ya mpambano

Safari ya ubingwa wa timu ya Mkoa wa Mtwara ilianzia hatua ya makundi ambapo walicheza mechi Nne na kushinda zote. Mechi hizo ni Pemba, Geita, Pwani na Mara.
baada ya kuvuka hatua ya makundi timu hiyo ilishinda mchezo wa robo fainali kati yake na timu ya Mkoa wa Lindi na kuiwezesha  kuingia nusu fainali kwa kucheza na timu ya Mkoa wa Mbeya na kuwafunga seti 3-1.
Timu ya Mkoa wa Mtwara pamoja na walimu wao muda mchache kabla ya kuanza kwa mchezo wa nusu fainali kati yake na timu ya Mkoa wa Mbeya.
Akizungumzia mashindano hayo Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara ameipongeza timu hiyo na kuahidi kuendeleza ushindi huo. Aidha, ameagiza walimu wote wa michezo mkoani Mtwara kuhakikisha wanawaandaa watoto katika michezo yote.
“Tumejifunza kilichotufanya tukashindwa kupata ushindi katika michezo mingine. Sasa ni suala la kujipanga kuhakikisha tunaondoa changamoto zote zinzazotukwamisha. Jambo la kwanza Walimu wa michezo wahakikishe wanawaandaa vizuri wanafunzi katika michezo yote.
Naye Mwalimu wa michezo wa volleyball Timu ya Mkoa wa Mtwara Gabriel Joshua ameshukuru vijana wake kwa kufuata maelekezo. Amesema tangu wanaandaa timu, lengo lao lilikuwa kuzishinda timu zote hasa timu ya mkoa wa Dar es salaam ambao wamekuwa washindani wao kwa kila mwaka.
“Mwaka jana hawa Dar es Salaam ndio walitutuoa fainali. Kwa hiyo tulijiandaa vema kuhakikisha hawapati nafasi hiyo tena.”
Joshua akiwa amebebwa na wanafunzi wake mara baada ya ushindi
Naye kapteni wa timu hiyo Mwanahawa Ezekiel wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mkalapa amesema wanafurahia kufikia hatua hiyo na kwamba wanajiandaa kuhakikisha wanaiwakilisha vema Tanzania katika mashindano ya Afrika mashariki.
Mwanahawa Elisha Ezekieli maarufu kama ‘Ngolo Kante’
Pongezi zingine za ushindi huo zimetolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara Bi, Germana Mung’aho. Licha ya kufurahishwa na matokeo hayo, Bi Mung’aho ameahidi kuhakikisha morali hiyo ya ushindi inaelekezwa kwenye michezo yote. Amesema ushindi huo umewapa tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya  Shule za Sekondari Afrika Mashariki (FEASA) yanayotarajiwa kufanyika jijini Arusha Agosti mwaka huu.
Germana Mung’aho. Mwenye jaketi Jeusi na fulana nyeupe katikati




No comments:

Post a Comment