MTWARA RS

FUATILIA TAARIFA MBALIMBALI ZINAZOHUSU MKOA WA MTWARA NA SEHEMU NYINGINE NDANI NA NJE YA TANZANIA, KWA MAWASILIANO E-mail: yustace.evaristy@mtwara.go.tz SIMU: +255 717 697 205

Monday 21 November 2016

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kuanza mwakani




Jengo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa mkoani Mtwara.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa eneo la Mitengo Mjini Mtwara inatarajiwa kuanza mwakani.  Hayo ameyasema leo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake  mkoani Hapa.



Mwalimu amesema bajeti iliyotengwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 kiasi cha bilioni mbili hazitoshi kukamilisha kila kitu lakini atahakikisha inapatikana fedha ya kutosha kwenye mwaka wa fedha wa 2017/2018 ili hospitali hiyo ianze mara moja.



‘Ahadi kubwa  ninayotoa kwenu Mtwara, Lindi na Ruvuma ni kuhakikisha tunatafuta fedha. Hatutategemea fedha za hazina tu, bali hata kutoka kwa wenzetu wa Bima ya Afya. Nawaahidi kuwa bajeti ya 2017/2018 hospitali hii itaanza kutoa huduma hata kama hatutaanza na huduma zote, lakini zile zinazowezekana zitaanza kufanyika’. Amesema Mwalimu.



Amesema haipendezi mgonjwa anatokea Mtwara, Ruvuma na Lindi kwa ajili ya kufuatilia huduma ya CT-Scan Dar es salaam Wakati hospitali hiyo ingekuwepo, huduma hiyo ingeweza kupatikana hapahapa.



Awali akiwasilisha maombi kwa Mheshimiwa Waziri, Mbunge wa jimbo la Nanyamba, Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota  amesema kukamilika kwa Hospitali hiyo iliyoazimiwa tangu vikao vya CCM vya  mwaka 1977 kutasaidia kupunguza adha kwa wananchi wa mikoa ya kusini ambao wamekuwa wakihangaika kwa kiasi kikubwa kutafuta Huduma za Matibabu jijini Dar es Salaam.



Chikota amesema kwa sasa wananchi wa Mikoa ya Mtwara wamekuwa wakihangaika kupeleka wagonjwa katika Hospitali ya Ndanda ambayo hata hivyo haina uwezo Mkubwa.



Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Wedson Sichalwe amesema amepokea kwa furaha kubwa kauli ya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na kwamba na kwamba hilo litasaidia kusogeza Huduma za Kibingwa karibu na wananchi.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mwenye vazi la Dela Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mtwara na Lindi. Mwenye T-shirt nyeupe katikati ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dr. Wedson Sichalwe



1 comment: